Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sikiliza kisa cha Jabir na baba mdogo

52893 Edo+Kumwembe

Thu, 18 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sikiliza nikusimulie kisa cha mfanyakazi wetu wa ndani, nyumbani kwa baba yangu mdogo pale Mwananyamala. Aliitwa Jabir. Alikuwa mfanyakazi wetu wa ndani ambaye aliibuka kuwa rafiki pia wa bosi wake.

Mama yangu mdogo alifariki mwaka 1994. Baba akaamua kutooa tena. Muda mwingi alikuwa anaishi na wafanyakazi wake na ndugu kadhaa. Jabir alitokea kuwa mfanyakazi aliyedumu sana kwa sababu alijua namna ya kuishi naye.

Baba mdogo alikuwa anapenda kinywaji. Angeweza kumaliza chupa mbili kubwa za konyagi bila ya shida. Kuna tukio lilikuwa linanichekesha sana wakati kilevi kilipokuwa kinamwingia kichwani. Mara kadhaa nilimkuta Jabir akimnyang’anya glasi. Woga dhidi ya bosi wake ulikuwa unamtoka. Sio kwa ujeuri.

Siku moja nikamuuliza kwa nini? Akanijibu “mara nyingi akilewa huwa anaziangusha. Asubuhi ananifokea mimi kwamba navunja glasi. Ni bora nimnyang’anye kwa sababu asubuhi hakutakuwa na kesi. Hatakumbuka chochote na idadi ya glasi itaendelea kuwa ile ile”. Nikamuelewa Jabir. Alikuwa anatumia akili ya kuzaliwa.

Hii ndio akili ambayo watendaji wetu wengi pia inabidi waitumie katika nyakati hizi ambazo wanasiasa wameendelea kuwa na nguvu nchini kuliko wataalamu. Wanasiasa wetu wamekuwa watu wa maagizo. Watu wa kauli kali. Hata kama hawajui hasa mambo ya kitaalamu.

Mambo yanapoharibika mara nyingi wanasiasa wanawalaumu watendaji. Wanasahau kauli zao za sifa ambazo hazikulenga weledi wa mambo (Professionalism). Tunapoelekea katika uchaguzi utaona tu jinsi ambavyo watendaji wanalaumiwa asubuhi kama Mzee Kumwembe alivyokuwa akimlaumu Jabir kwa glasi alizovunja mwenyewe.

Mwanasiasa hakumbuki kama alivunja ‘glasi’. Wakati anavunja anakuwa amelewa madaraka. Anasahau kwamba siku moja atauliza ni nani aliyevunja. Nimeanza kuona kauli za wanasiasa wetu katika siku za karibuni. Wameanza kuutupa mzigo wa ‘uvunjwaji’ wa glasi kwa watendaji.

Watendaji wasimeze kila kitu wanachoambiwa licha ya ubosi wa wanasiasa. Kama wanaweza wawanyang’anye glasi mapema wanasiasa. Kisa cha Jabiri huwa kinanikumbusha mengi sana. maslahi ya nchi ni muhimu kuliko kauli za wanasiasa. Huwa natembea na kisa cha Jabir kila ninapokwenda kufanya kazi mahala. Kinanichekesha sana, lakini ndio ukweli halisi.



Chanzo: mwananchi.co.tz