Dar es Salaam. Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (Sido) limetakiwa kuelekeza nguvu zake kuwapatia wajasiliamali mashine za uzalishaji pamoja na mafunzo na sio fedha taslimu ili kuwawezesha kuanzisha viwanda vidogo katika maeneo wanapoishi na kuwajengea uwezo wa kiuchumi.
Akizungumza wakati akizindua bodi mpya ya shirika hilo juzi, Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda alilitaka shirika hilo kuwapatia mashine na mafunzo wajasiliamali na linaweza kuingia ubia na mjasiliamali na kupata faida.
“Inashangaza kuona mjasiriamali amekopa fedha za kusindika matunda lakini badala yake anafanya vitu vingine ambavyo havina faida na kusababisha hasara kubwa.”
“Faida ambayo Sido itapata kutoka kwenye ubia na wajasiliamali itasaidia kwa kiasi kikubwa shirika kukua kwa haraka na kufikia uwezo wa kutoa gawio kubwa kwa Serikali,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Sido, Profesa Sylvester Mpanduji alisema shirika hilo linaendelea kuwa muhimili mkuu wa Serikali katika kuendeleza viwanda, biashara ndogo na za kati kwa lengo la kuchangia katika kuondoa umasikini na kukuza maendeleo ya nchi.