Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sheria ya manunuzi na madudu yake

Cag Kichere Gh Sheria ya manunuzi na madudu yake

Mon, 3 Apr 2023 Chanzo: Habarileo

WACHAMBUZI wa masuala ya uchumi na siasa wameishauri serikali ifanye tathmini ya sheria ya ununuzi, mifumo ya maadili ya utumishi wa umma na mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa kuwa vinachangia wizi wa fedha za miradi.

Pia wameshauri wabadhirifu wa fedha za umma watangazwe hadharani kwa kuwa kuendelea kuwaficha ni sawa na kukubali tatizo liendelee.

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alikerwa na nyongeza ya malipo kwenye utekelezaji wa miradi ya serikali ukiwamo ununuzi wa ndege ya mizigo ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).

Rais Samia alisema kwenye ununuzi wa ndege hiyo kuna nyongeza ya malipo kutoka Dola za Marekani milioni 37 hadi Dola za Marekani milioni 86.

Aliagiza wote walioshiriki kuongeza fedha hizo waondoke kwa kuwa hawafai kuendelea kuwepo serikalini.

Mchambuzi Abbas Mwalimu anasema mifumo ya maadili nchini ina changamoto kuanzia ngazi ya familia, makundi rika, taasisi za dini, taasisi za elimu ambako kuna wizi wa mitihani na wanafunzi kuingia na vikaratasi kwenye mitihani.

Mwalimu alisema watu hao baadaye wanapata fursa ya kuongoza ofisi za umma au serikali, hivyo kwao kujihusisha na ubadhirifu wa mali za umma haitakuwa tatizo.

“Tunayo Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995, lakini haina ‘effect’ (matokeo) kwa sababu tayari huyu mtu ameshaathirika tangu mwanzo, pia tuna sheria ya utumishi wa umma ya mwaka 2002 ilifanyiwa maboresho mwaka 2019, lakini zimekuwa hazina nguvu katika kuchukua hatua stahiki,” alisema.

Mwalimu ameshauri Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ipewe mamlaka kisheria ya kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa ubadhirifu wa fedha za serikali.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Magdalena Sakaya amedai kuwa asilimia 80 ya fedha za Watanzania zinaliwa kwenye ununuzi unaofanywa na maofisa wa serikali.

Sakaya akasema hakuna mradi wa serikali ambao hauna ununuzi na licha ya kuwa na sheria ya ununuzi wabadhirifu hupitia humo humo kwenye sheria kutekeleza uhalifu wao.

“Kwanza kwa sehemu kubwa sheria hiyo haifuatwi, hata kama inafuatwa wanachokifanya wanatangulia kwa wafanyabiashara, kwa mfano bei ya soko ya bati ni Sh 5,000, anamwambia mfanyabiashara afanye Sh 8,000, sasa piga hesabu ya Sh 8,000 kwenye idadi ya mabati yatakayonunuliwa, kwa hiyo hapo ana Sh 2,000 za kwake na anamwachia mfanyabiashara aliyemwandaa Sh 1,000,” alisema Sakaya na kuongeza:

“Huu ni mfano mdogo tu wa bati, lakini mradi huo una matofali, mbao, rangi, misumari, sasa anataka ale kwenye kila bidhaa, kwa hiyo licha ya serikali kuamua miradi isimamiwe na watumishi wa umma, lakini matokeo yake baadhi wametajirika huko huko.”

Akamshauri Rais Samia aunde chombo maalumu katika kila mkoa na wilaya ambacho kitakuwa jicho lake kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa miradi.

Mchambuzi mwingine, Walter Nguma akadai kuwa asilimia 80 ya wizi wa fedha za umma unafanyika kupitia ununuzi na asilimia 20 iliyobaki kwenye mikataba ambayo serikali inaingia na wakandarasi.

“Pengine utoaji wa fedha sasa hivi kutoka serikalini kwa ajili ya manunuzi umekuwa mwepesi kiasi kwamba watu wanaona hata uongeze sifuri kiasi gani, fedha hiyo italipwa. Haya ni makosa makubwa, tuna shida katika mfumo wa manunuzi na mfumo mzima wa ulipaji wa vyeti kwa kampuni zinazotekeleza miradi ya serikali,” alisema Nguma.

Rais wa Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA), Godvictor Lyimo anasema ili kudhibiti wizi wa fedha za umma serikali inapaswa kubadili mfumo wa kuwapata wasimamizi wa miradi.

“Pia kuwe na mifumo ya kuwawajibisha wabidhirifu na wasio na weledi, kwenye Bodi za Wakurugenzi pia watu wapatikane kwa njia ya ushindani badala ya kuwateua ili kuleta tija,”alisema Lyimo.

Akashauri kuimarisha mifumo ya usimamizi na sheria ili kila mtu atimize wajibu wake.

Chanzo: Habarileo