Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sheria ndogo za wamachinga kutafsiriwa kwa Kiswahili

Chinga Boys Wiki ya wamachinga ufanyika Juni 29 kila mwaka.

Mon, 28 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Shirikisho la Umoja wa Wamachinga (SHIUMA) imeazimia kuhakikisha sheria ndogo zinazowahusu wamachinga zinatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili Wamachinga wote waweze kuzielewa.

Maazimio hayo yamefikiwa wakati wa kuhitimisha kikao cha siku mbili kati ya wizara na viongozi wa SHIUMA kutoka Mikoa ya Tanzania Bara kilichoongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk Zainab Chaula kilichofanyika Jijini Dodoma.

Akifunga kikao hicho, Dk Chaula amewataka Wamachinga kushirikiana na Serikali kutekeleza maazimio waliyojiwekea kwa wakati kwa maslahi yao na Taifa kwa ujumla.

"Kufikia tarehe 16 Machi wanasheria wa SHIUMA kwa kushirikiana na wanasheria wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Ofisi ya Rais TAMISEMI wakamilishe kutafsiri Sheria hizo," amesema Dk Chaula.

Dk Chaula ameyataja maazimo ya kikao hicho kuwa ni pamoja na wizara yke iboreshe madawati ya kushughulikia masuala ya Wamachinga kwa kushirikiana na Ofisi Rais Tamisemi hadi halmashauri ili kusaidia kutatua changamoto kwenye maeneo yao.

Pia wizara kwa kushirikiana na Tamisemi kuhakikisha mamlaka za Serikali za mitaa zinapanga na kuweka miundombinu wezeshi katika maeneo ya shughuli za Wamachinga kwa kushirikiana na Viongozi wa Wamachinga wa eneo husika.

Azimio lingine ni kuandaa kanzidata ya Wamachinga na wizara kutembelea maeneo ya masoko ya Wamachinga ili kutatua changamoto zilizopo.

Mwenyekiti wa SHIUMA Taifa, Ernest Matondo ameishukuru Serikali kwa kuwakutanisha Wamachinga na kuahidi kushirikiana na viongozi pamoja na Wamachinga mikoa yote ili kufanikisha kufika mbali na kutoka katika umachinga na kuwa wafanyabishara wa kati na wakubwa.

​Aidha, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na SHIUMA imeanza mikakati ya kuratibu maadhimisho ya wiki ya Wamachinga itakayofanyika Juni 29 kila mwaka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live