Sheria zaidi ya 24 zimerekebishwa na nyingine 18 zinafanyiwa kazi zirekebishwe kwa lengo la kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali nchini katika Serikali ya Awamu ya Sita.
Katibu Mkuu wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Profesa Godius Kahyarara alisema hayo wakati wa majadiliano na nchi za Nordic ambazo ni Denmark, Finland, Sweden na Norway, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini Tanzania (REPOA).
“Kulikuwa na kero nyingi, tozo nyingi zimefutwa karibia 232 si kitu cha mchezo…Tunaangalia taasisi ambazo miundo imebadilishwa ni zaidi ya 57, hizo ni hatua zinazochukuliwa na serikali ili kuweka mazingira bora katika uwekezaji,” alisema.
Alisema kutokana na jitihada hizo katika kipindi cha mwaka mmoja cha awamu ya sita, mauzo ya nje yamepanda. “Tulikuwa tuna export (kusafirisha nje) Dola bilioni saba mpaka nane lakini sasa tumefika Dola bilioni 10 na tunaenda mbele zaidi,” alisema.
Awali, alisema nchi hizo za Nordic zinafurahia mageuzi makubwa ya uchumi nchini ikiwamo kuongezeka kwa uwekezaji pamoja na kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara pamoja na kukua kwa ushirikiano wa kiuchumi.
Alisema nchi hizo zimeona ni kwa kiasi gani serikali imebadili mtazamo wa dunia na mwelekeo wa uchumi kwa Tanzania.
Alisema mapato yameongezeka kwa asilimia 20 ikilinganishwa na awamu iliyopita. Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari alisema nchi za Nordic zina mashirika makubwa yanayoshirikiana na Tanzania katika uwekezaji.
Alisema maeneo yaliyokuwa na changamoto waliyoyabaini na kukabidhi ripoti serikalini, imani yao ni kwamba yataongeza uwekezaji wa Tanzania na nchi hizo.
Alisema hivi sasa hapa nchini zipo bidhaa zinazalishwa kwa kukidhi viwango vya kimataifa. Alisema bidhaa kama nguo hapa nchini zipo zinazozalishwa kwa kukidhi masoko ya nje.
Naye Balozi wa Sweden nchini, Anders Sjoberg alisema kwa kuwa serikali ya Tanzania imefungua milango kwa wawekezaji na kwamba nchi za Nordic zipo tayari kusaidia ushirikiano uliopo kwa njia yoyote kuhakikisha mabadiliko makubwa yanakuwepo.