Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shehena ya parachichi yaelekea India

Avocado 878958 1920 1140x640 Shehena ya parachichi yaelekea India

Sat, 22 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shehena ya pili ya matunda aina ya parachichi imeondoka usiku wa jana kuelekea nchini India katima hatua za kuyatafutia masoko matunda na mazao yanayolimwa nchini.

Naibu waziri wa kilimo Anthony Mavunde alikua mmoja kati ya walioshuhudia mzigo huo ukiondoka nchini.

“Leo usiku tarehe 21 Januari, 2022 nikiwa na Balozi wa India nchini Tanzania, Mheshimiwa Binaya Srikanta Pradhan tumeshuhudia usafirishaji wa parachichi kuelekea nchini India kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikiwa ni mzigo wa pili unaokamilisha tani 2.2 tangu parachichi ianze kusafirishwa Januari,2022.” Alisema Mavunde.

Mavunde alisema tukio hili ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Viongozi wakuu wa Nchi akiwemo Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025 ambayo imeielekeza serikali kutafuta masoko ya mazao ya wakulima ndani na nje ya nchi.

Ameongeza kuwa, Tanzania kwa sasa inazalisha wastani wa tani 40,000 za parachichi ambapo ni tani 9,500 pekee ambazo zinauzwa nje ya nchi.

Aidha alisema nchi ya Tanzania ina fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji wa parachichi, ikiwa uhamasishaji utaendelea kuhamasisha wakulima kuzalisha kwa tija na kufuata kanuni za kilimo bora.

Mavunde aliongeza kuwa kupitia bajeti ya mwaka ujao wa fedha, Wizara imedhamiria kuanzisha Kituo Maalum kati ya Mkoa wa Iringa na Njombe ambapo, Kituo hicho kitafanya kazi ya kukusanya parachichi, kuchambua kwa kupanga madaraja na kuhifadhi kwenye vifungashio vyenye lebo ambayo itakuwa inaonesha uasili wa bidhaa hiyo, hali ambayo itasaidia kuongeza wigo wa masoko ya parachichi, tofauti na sasa ambapo parachichi asilimia kubwa inatoroshwa na kuuzwa nje kama bidhaa isiyotoka Tanzania

“Mkakati mwingine tuliodhamiria kama Wizara ni kuanzisha Mnyororo wa Kijani (Green channel) kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wa mazao ya horticulture kuanzia shambani mpaka yanapofika kwenye kituo cha kusafirishia kwenda nje ya nchi.” Alisema.

Tayari Wizara ya Kilimo imeanza kufanya mazungumzo na Wadau mbalimbali wakiwemo Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi; Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi; Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Sekta binafsi kwa lengo la kuhakiksha mfumo huo endelevu wa mnyororo wa kijani au Green Channel unaanzishwa nchini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live