Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sh55 bilioni za SDC kuboresha ufundi stadi nchini

Fri, 31 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC), limesema litachangia Sh55 bilioni kwa kipindi cha miaka 12 kwa ajili ya kusaidia kuboresha maendeleo ya ufundi stadi Tanzania.

Balozi wa Uswisi Tanzania, Florence Mattli ameeleza hayo alipokuwa akizindua awamu ya kwanza ya programu ya Stadi za Ajira Tanzania (SET) inayofadhiliwa na ubalozi huo.

Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.

Mattli amesema programu  hiyo inakwenda sambamba na  Mkakati wa Taifa wa  Tanzania wa  Stadi za Ufundi, unaolenga kuimarisha uwezo wa kitaifa wa Mfumo wa Maendeleo ya Stadi za Ufundi (SDV) na kukuza fursa za maendeleo ya stadi zinazotokana na mahitaji ya ajira na itatekelezwa na shirika la Swisscontact.

“SET itaboresha matarajio ya ajira ya kujiajiri na kuajiriwa, kwa kuchangia upatikanaji, umuhimu na ubora wa mafunzo ya ufundi stadi.

“Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema; “ili maendeleo ya kweli yaweze kupatikana  ni lazima watu washirikishwe, katika programu hii tunashirikiana na mashirika yenye utaalamu na eneo husika, ”amesema.

Pia Soma

Amesema watatumia taasisi za Kitanzania sanjari na kuunganisha juhudi zetu na zile za wadau muhimu hasa sekta binafsi.

Kwa mujibu wa Mattli, programu ya SET inawalenga vijana wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 24 hasa wale ambao bado hawajafikiwa na mfumo rasmi wa Maendeleo ya Ufundi Stadi (VSD) ikiwa ni pamoja na wasichana.

 Programu hiyo itafanya kazi kwa ukaribu na mamlaka za elimu na mafunzo ya ufundi stadi na taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Kwa upande wake, Profesa Ndalichako amesema katika fedha hizo, Sh15bilioni zitakwenda kuboresha mafunzo ili kuwawezesha wakufunzi wa masomo ya ufundi kuwa na mtizamo wa ujasiriamali utakaowasaidia wanafunzi wanaowafundisha.

“Katika huu mradi tutaboresha mafunzo katika vyuo vya maendeleo ya wananchi 16 ili yaendane na teknolojia ya kisasa. Kutakuwa na kompyuta na programu zitakazoendana na hali halisi ya soko la dunia kwa sasa,” amesema Profesa Ndalichako.

Chanzo: mwananchi.co.tz