Serikali imepanga kuiwezesha Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kwa kuipatia mtaji wa takribani Sh40 bilioni utakaoiwezesha kununua na kusambaza mbolea kwa wakulima.
Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde wakati akijibu swali la msingi leo Alhamis Juni 22, 23 la Mbunge wa Iringa Mjini (CCM) Jesca Msambatavangu ameeleza.
Amesema Serikali inaendelea kushirikiana na Sekta binafsi vikiwemo viwanda vya Minjingu Mines and Fertilizer Limited na Itracom Fertilizers Limited kuhakikisha uzalishaji na upatikanaji wa mbolea hapa nchini unaimarika na kupunguza utegemezi wa kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi.
“Kupitia mpango huo, uwekezaji unaofanywa na kiwanda cha ITRACOM unatarajiwa kufikia uzalishaji wa takribani tani 1,000,000 za mbolea kwa mwaka ifikapo Desemba 2024,”amesema.
Amesema kiwanda cha mbolea cha Minjingu kinafanya upanuzi ili kuongeza uwezo wa uzalishaji kutoka tani 100,000 hadi kufikia tani 300,000 kwa mwaka.
Katika msimu wa 2023/2024 Serikali imepanga kuiwezesha Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kwa kuipatia mtaji wa takribani Sh40 bilioni utakao iwezesha kununua na kusambaza mbolea kwa wakulima.
“Serikali kwa kushirikiana na kampuni za mbolea na Vyama vya Ushirika imepanga kuongeza vituo vya mauzo ya mbolea nchini ili kuwezesha wakulima kupata mbolea kwa urahisi na kwa wakati,”amesema.