Zaidi ya Sh14 bilioni zitatumiwa na kampuni ya uwekezaji ya Panda Hill kwa ajili ya kuhamisha gereza la Kilimo la Songwe Mkoa wa Mbeya kupisha mradi wa uchimbaji madini ya Niobium yanayotumika kutengeneza injini za ndege, magari na vyuma vya kujenga madaraja .
Mwakilishi wa Kampuni hiyo, Emmanuel Kisasi amesema hayo leo Jumapili June 26,2022 wakati wa Kongamano la wadau wa Sekta ya Nishati na Madini lililoliandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera na kufunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Saimon Mayeka.
Kisasi amesema nyumba 120 za Jeshi la Magereza na wafungwa 600 watahamishwa kupisha mradi huo.
''Tayari hatua za awali tumeanza na sasa tupo kwenye mazungumzo na Serikali ili kuanza utekelezaji wa mradi ambao utatoa ajira 850 na asilimia 54 za manunuzi ya bidhaa yatafanyika nchini” amesema
Ameeleza mkataba wa uchimbaji wa madini hayo utadumu kwa miaka 30 huku Serikali ikitarajia kupata mapato ya Dola 600 milioni kwa mwaka.
Kwa upande wake Kamishna msaidizi wa Magereza na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya , Adriano Mduda amekiri kuwepo kwa uwekezaji huo na kubainisha kuwa hautoathiri katika eneo la mashamba yanayozalisha mazao na ufugaji katika eneo hilo la gereza.
Akifungua Kongamano hilo Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Saimon Mayeka amesema lengo ni kujenga uelewa wa pamoja na kuhamasisha mtandao wa kibiashara ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kubaini changamoto zinazowakabili na kuzitatua.
Naye, Katibu Tawala Msaidizi uchumi na uzalishaji mkoani humo ,Said Madito amesema wamelenga Sekta ya Nishati na Madini kutokana na mchango wao mkubwa.