Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria leo jumatatu Aprili 24,2023 imesema Serikali imelipa Sh1.07 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa makazi na ofisi za Makamu wa Rais kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Kauli hiyo, imetolewa na Mbunge Edward Olelekaita wakati akisoma taarifa ya kamati hiyo kwa niaba ya mwenyekiti kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na maoni ya kamati hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo 2023/2024.
“Kwenye mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya Sh1 bilioni ilitumika kwa ajili ya ukarabati wa makazi ya Makamu wa Rais, kilimani-Dodoma, Oystebay-Dar es Salaam na Ofisi ya Makamu wa Rais Luthuli 2- Dar es Salaam,”amesema.
Aidha, Olelekaita amesema hadi Machi 2023, kiasi cha Sh991.4 bilioni kililipwa kwa mkandarasi kwa ajili ya kazi zilizofanyika Kilimani-Dodoma na Oysterbay-Dar es Salaam kwenye makazi na ofisi za Makamu wa Rais. Kazi hizo ni pamoja na ujenzi wa ukuta, ujenzi wa nyumba na mapumziko kwa ajili ya madereva na miundombinu mingine.
Olelekaita ameongeza kuwa Sh87.9 milioni zilitumika kufanyia marekebisho ya ofisi ya Makamu wa Rais iliyopo Luthuli 2- Dar es Salaam.
“Fedha hiyo imetumika katika uzibaji wa nyufa, ukarabati wa dali, kupaka rangi ndani na nje ya ofisi, kuweka mifumo ya zimamoto, kuweka mfumo wa maji taka na safi, kukamilisha uzio, kukarabati milango, ngazi na geti la kuingilia.
Pia, amezitaja kazi ambazo zipo katika hatua ya awali ni matengenezo ya sehemu ya kuegeshea magari katika ofisi hiyo ya Luthuli 2 iliyopo jijini Dar es Salaam.
Bunge linaendelea na shughuli zake ikiwa ni mkutano wa kumi na moja kikao cha 12, ambapo mapendekezo ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2022/2023.