SERIKALI imetenga Sh bilioni 60 kuboresha miundombinu ya bandari 15 zilizopo kwenye mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa zinazosafirisha mizigo kwenda nchi za Afrika Mashariki.
Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa Kanda ya Ziwa Victoria mkoani Mwanza, Fernand Nyathi amesema hayo Agosti 30, 2023.
Nyathi alisema kwa Kanda ya Ziwa kuna bandari sita kubwa na ndogo tisa katika mikoa mitano ya Shinyanga, Mwanza, Mara, Kagera na Simiyu na fedha hizo zimeanza kufanya maboresho ambapo Bandari ya Ziwa Victoria Kaskazini imetengewa Sh milioni 18.6 na imeanza kukarabatiwa ikiwemo jengo la wasafiri.
“Waandishi wa habari mtakuwa mabalozi wazuri na kuelimisha umma hivyo serikali imeweka fedha kwaajili ya kukarabati bandari hizi ikiwemo ya Kemondo hivyo matarajio yatachochea ukuaji wa uchumi kwa uingizaji wa mizigo kutoka kwenye nchi za Afrika Mashariki.” alisema.
“Tunatarajia kuongezeka kwa shehena kwa kiwango kikubwa na Meli kwani changamoto iliyopo ni uchakavu wa miundombinu kuja kwa uchache wa mizigo lakini kwa mwaka wanauwezo wa kupokea tani 3000.” aliongeza Nyathi..
Meneja wa bandari kavu ya Isaka, Abel Mshang’a alisema wanapokea mizigo kwa njia ya reli ambapo kilijengwa mwaka 1995 na kuanza rasmi mwaka 2017 kutoa huduma za kibandari na uwezo wa kuchukua makasha 300 hadi 350 yenye urefu wa futi 40 na uwezo wa kuchukua makontena 22 kwa muda mmoja.
“Bandari ya Isaka ni kurahisisha mizigo kufika kwa haraka watumiaji wa bandari wanapata manufaa makubwa ya kusafirisha mizigo pasipo na shaka na hurudishwa kasha likiwa tupu bure baada ya mzigo uliobebwa kutolewa na wananchi wanaozunguka eneo la bandari wanafaidika kutoa huduma mbalimbali na kukuza uchumi wao.”alisema Mshang’a.
Mkuu wa kituo cha reli ya kati Isaka Zacharia Mwantunge alisema wamekuwa wakipokea mizigo kama ngano kutoka Dar es salaam kwenda Rwanda, Nakuru, Congo na wamekuwa wakipokea mizigo midogomidogo ya mahindi na mpunga kwa wananchi wa kawaida kutoka Katavi na Mpanda.
“Katika makasha 57 yaliyohudumiwa mwezi huu na Shirika la Reli ni Makasha 17 ya mabomba ya mafuta yaliyokuja kwa njia hiyo hivyo bado kuna manufaa makubwa ya utumiaji wa reli na Bandari kwa masaa 24 ikifanya kazi.”alisema Mwatunge.