Ujenzi wa Soko la Ndizi la Urafiki lililopo Halmashauri ya Ubungo mkoani Dar es Salaam umeanza rasmi, muda mchache baada ya uongozi uliokuwepo kuondolewa
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Hashim Komba amesema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLeo kuhusu ujenzi wa soko hilo ambalo awali lilimilikiwa na wafanyabiashara lakini sasa hivi limerudishwa serikalini.
Komba amesema sh milioni 600 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi katika Soko hilo ambao tayari umeanza na jengo la kwanza.
“Na kwa kuanzia imeshatengwa bajeti milioni 600 ambayo ndio inaanza kwa ajili ya kufanya maboresho na ukienda sasa hivi eneo lile ambalo wanauza ndizi utakuta tayari kuna jengo limeanza kujengwa la kwanza kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara waanze kukaa kwenye maeneo mazuri,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Ameeleza baada ya jengo hilo kukamilika ujenzi utaendelea kwenye majengo mengine pamoja na choo cha kisasa, ujenzi wa mitaro kwa ajili ya kuchepusha maji na eneo la maegesho ya magari.
Amesema ujenzi unaoendelea utasaidia kwa kuwa kipindi cha mvua wafanyabiashara wamekuwa wakifanya biashara kwenye matope, biashara zinakuwa juu ya matope na wateja wanaingia na kukanyaga matope.
Ameongeza endapo soko lingekuwa wazi ujenzi ungeenda haraka zaidi lakini kwa kuwa wanajenga huku biashara zinafanyika lazima ukamilishe eneo moja unawahamisha wafanyabiashara kwenye eneo ambalo limekamilika huku ukibomoa eneo lingine kwa ajili ya kufanya maboresho.