Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yawekeza umwagiliaji uongeze ajira 120,159

35797e84fe68d8570e4b261776ee6e64 Serikali yawekeza umwagiliaji uongeze ajira 120,159

Fri, 19 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali sekta ya umwagiliaji katika mikoa saba nchini utaongeza kiwango cha uzalishaji wa mazao pamoja na kuimarisha sekta ya ajira nchini.

Bashe alisema hayo hivi karibuni katika kilele cha maadhimisho ya maonesho ya wakulima na wafugaji maarufu Nanenane mkoani Mbeya na akasema sekta ya umwagiliaji itaongeza ajira zaidi ya 120,159.

Alisema ongezeko la bajeti ya sekta ya umwagiliaji kutoka Sh bilioni 57 hadi bilioni 416 mwaka huu limetokana na ongezeko la bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan ambapo jumla ya miradi 21 yenye ukubwa wa hekta 26,700 yenye thamani ya Sh bilioni 182 inatekelezwa na mikataba imeshasainiwa.

Bashe alisema utekelezaji wa miradi hiyo 21 utafanya bajeti ya umwagiliaji kutekelezwa kwa zaidi ya asilimia 51 na kuongeza kuwa miradi hiyo ya umwagiliaji itaongeza kiwango cha uzalishaji hadi kufikia tani 97,300 za mchele.

“Mheshimiwa Rais, katika phase hii inayojengwa sasa hivi, tutajenga mabwawa makubwa matatu ambayo yatakuwa na ujazo wa mita za ujazo milioni tisa na pia yatakuwa na miundombinu ya kunyweshea mifugo ili kuzuia wafugaji wasiingie katika mashamba ya wakulima,” alisema.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na wanahabari mkoani Tabora hivi karibuni kuelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali alisema serikali iliamua kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Sh bilioni 294 mwaka jana hadi bilioni 954 ili kubadilisha maisha ya wakulima na kuongeza uzalishaji wa mazao nchini.

Alisema serikali imeweka kipaumbele katika kilimo cha umwagiliaji ili kutoa fursa sawa kwa Watanzania waweze kunufaika kutokana na kilimo na kutoa rai kwa vijana badala ya kubanana mijini waende kunufaika na fursa iliyotolewa na serikali.

“Nitoe wito kwa vijana badala ya kubaki mijini na kulalamika kuwa hakuna ajira fursa hii ya bilioni 954 imepelekwa vijijini kwenye maeneo ya kilimo, twendeni tukachangamkie fursa tulime na serikali imeahidi kuwa wakulima mkilima mazao yenu hakuna atakayewapangia mahali pa kuuza,” alisema Msigwa.

Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025 ukurasa wa 34 inasema chama kitaendelea kuhakikisha kuwa Taifa linajitosheleza kwa akiba ya chakula na kuwa na wastani wa asilimia 121.1 mwaka 2015 - 2020 ikilinganishwa na asilimia 114.6 mwaka 2010 – 2015. Ilani hiyo imetaja skimu za umwagiliaji 135 zikiwemo zile za Mforo (Mwanga), Hanga - Ngadinda Madaba na Skimu ya Igongwa iliyopo katika Halmashauri ya Misungwi huku upembuzi yakinifu na usanifu wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu za Luiche (Kigoma Ujiji), Ibanda (Sengerema/ Geita) na Gidahababieg (Hanang) pamoja na zingine 22 umekamilika.

Ukarabati wa ekari 2,000 za skimu kubwa ya Dakawa pamoja na barabara zake na mafunzo ya uongezaji tija kufikia zaidi ya tani 7 kwa hekta umefikiwa ambayo ni kati ya tija za juu duniani.

Ukarabati na ujenzi wa bwawa la Usoke (Urambo), bwawa la Itagata (Halmashauri ya Wilaya ya Itigi) na bwawa la Dongobesh (Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu) umekamilika pamoja na kuongezeka kwa eneo la umwagiliaji kwa ekari 30,130 na hivyo kufikia ekari 1,187,630 mwaka 2019.

Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2021/22- 2025/26) katika ukurasa wa 84 na 85 unabainisha kuwa sekta ya kilimo inaendelea kuwa kitovu cha ukuzaji wa viwanda na maisha ya watu nchini, ambapo inakadiriwa kuwa asilimia 58.1 ya watu wanapata kipato kutokana na shughuli za kilimo.

Mpango pia umeelekeza kuwa kwa kipindi chote cha utekelezaji wake, juhudi zitaelekezwa katika kuunganisha na kuimarisha mafanikio yaliyopatikana na kuzingatia fursa zinazopatikana kutokana na mbinu bora za kilimo zinazozingatia hali ya hewa kwa kufanya yafuatayo:-

Kufungamanisha sekta ya kilimo na sekta nyingine za kiuchumi, kujenga mazingira mazuri kwa sekta binafsi kuendesha shughuli za uzalishaji na uuzaji nje wa malighafi za kilimo na bidhaa zilizochakatwa.

Kwa mujibu wa mpango huo, hatua hizi zitaongeza thamani na tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo, kuzalisha ajira, kutanua wigo mseto wa bidhaa na kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live