Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaweka mazingira uchumi shirikishi wa dijiti

Uchumi Uchumiiii (600 X 300) Serikali yaweka mazingira uchumi shirikishi wa dijiti

Fri, 25 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imesema inaweka mazingira sawa kwa ajili ya ujenzi wa uchumi shirikishi wa kidijiti wenye fursa sawa kwa vijana na wanawake.

Kauli hiyo ilitolewa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa kwanza wa mwaka wa wanachama wa Tanzania Startup Association (TSA) uliofanyika Dar es Salaam juzi.

“Kwenye hili sio maneno, bali tayari tumeanza utekelezaji. Kama mmeona tayari tumetangaza tenda (zabuni) kwa ajili ya kupata wataalamu ambao wataisaidia Wizara kutengeneza mkakati wa uchumi wa kidijitali, pia kupata mtaalamu ambae atafanya uchambuzi wa sera, sheria na kanuni zetu zote zinazohusu TEHAMA,” alisema Nape.

Akifafanua zaidi Waziri Nape alisema kwa sasa kuna mchakato unaendelea chini ya Tume ya TEHAMA wa kuweka taratibu za utumiaji wa Tehama katika kufanikisha uanzishaji wa bidhaa katika mtandao na ubunifu salama ambao haingilii mifumo iliyopo ya mtandao.

Alisema kwa kuwepo kanuni na sheria hizo kutasaidia mawazo mapya na bunifu mbalimbali kufanyiwa majaribio kwenye soko kwa uangalifu maalumu mpaka hapo leseni rasmi zitakapotolewa.

Alisema utafiti uliofanywa hivi karibuni na taasisi ya TSA unaonesha wabunifu wa bidhaa ndani ya Tehama (Startups) wa Tanzania kwa wastani wanaweza kuzalisha ajira rasmi na zilizokuwa sio rasmi 133 kwa kila kampuni moja .

Aidha alisema ili kusaidia kushamiri kwa watu hao,Wizara yake hivi karibuni kupitia TCRA imeanza kutoa huduma ya USSD Codes bure kwa Startups na wabunifu, ambao hapo kabla walitakiwa kulipa takribani Dola za Marekani 3000 ili waweze kuzipata, ili wajaribu biashara zao.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inaamini na kuunga mkono kwa vitendo ujasiriamali, ubunifu na uchumi wa kidigitali ili kutatua changamoto za kijamii, kukabiliana na ukosefu wa ajira, kukuza uchumi na kuliltea sifa taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Startup Association, Zahoro Muhaji alisema tangu kuanzishwa kwa TSA, pamoja na mafanikio mengine imeweza kujenga uaminifu na mahusiano mazuri ya kiutendaji na serikali, kuwezesha kuondolewa kwa ada ya majaribio ya rasilimali za mawasiliano na TCRA na mchakato unaoendelea wa kuanzisha mifumo ya kisheria wa ajili ya Startup nchini.

Tanzania Startup Association (TSA) ni asasi ya wanachama isiyo ya faida inayowaleta pamoja wadau wa mfumo ikolojia wa kampuni changa za kibunifu Tanzania na aina nyingine za ujasiriamali wa kibunifu wa uvumbuzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live