Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yawapa somo wenye viwanda kuhusu taka rejereshi

Thu, 31 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wamiliki wa viwanda nchini wametakiwa kuhakikisha taka laini na ngumu wanazozalisha kupitia viwanda vyao wanazirejeresha ili zitumike kutengeneza uchumi endelevu wa nchi.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 30, 2019 na Mkurugenzi Mtendaji wa TanTrade, Edwin Rutegaruka kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Innocent Bashungwa, wakati akizindua mkutano wa mwaka wa pili wenye kauli mbiu ‘Biashara nzuri yenye kuchochoea Uchumi endelevu.’

Amesema wenye viwanda nchini wanatakiwa kuzingatia mambo makubwa matatu ikiwemo kufikiria namna gani wana madhara katika kuharibu mazingira.

“Kwa hiyo kila anayezalisha afikirie ni madhara gani yanayoweza kutokea katika jamii, la pili wafikirie ninapozalisha taka hizi laini au ngumu ambazo zinaweza kuleta madhara kwa binadamu je ninaweza vipi nikazitumia taka ngumu hizi au laini kutengeneza bidhaa,” amesema.

Rutegaruka amesema wamiliki wa viwanda lazima wafikirie kurithisha vizazi vijavyo,  “mtoto tangu anapokuwa shule ya msingi ajue kuwa taka zinaweza kuzalisha uchumi, Waziri ametoa wito kwa wadau wote waweze kujiunga na global Compact ili tushirikiane na wenzetu hawa wa jumuiya ya kimataifa katika kuhakikisha taka zetu zinabaki kuwa salama taka tunazozalisha viwandani, majumbani mwetu zinatumika katika kutengeneza uchumi endelevu wa nchi yetu,” amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz