Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yawaita mezani wanunuzi wa korosho

34044 Korosho+pic Tanzania Web Photo

Mon, 31 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati taarifa ya timu ya pamoja ya wataalamu kuhusu hali ya utekelezaji wa operesheni korosho iliyotolewa Novemba 27 ikionyesha kuwa itachukua kati ya miaka miwili hadi 14 kubangua korosho za msimu huu, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda amewakaribisha wafanyabiashara kununua korosho na kuzibangua.

Mbali na hatua hiyo, Waziri Kakunda amesema Serikali inaendelea kuingia mikataba na wabanguaji ili kupunguza mzigo wa korosho.

Novemba 12, Rais John Magufuli alitangaza Serikali kununua korosho yote kutoka kwa wakulima msimu huu kwa bei ya Sh3,300 kwa kilo huku.

Licha ya Waziri Kakunda kusema haina shida kwa ubanguaji kuchukua muda mrefu, amewataka wafanyabiashara wanaoweza kubangua wenyewe wakae meza moja na Serikali ili wauziwe korosho.

“Kama mtu anatokea popote iwe ndani au nje akasema mimi nataka ninunue korosho nikabangue mwenyewe, labda ana bei nzuri aje tuzungumze. Ije mvua, lije jua korosho ziko kwenye maghala, kuna tatizo hapo? Zitabanguliwa tu muda wowote,” alisema.

Alisema ubanguaji unaendelea baada ya Serikali kuingia mkataba na baadhi ya kampuni.

“Leo (juzi) ilikuwa niende kuzindua ubanguaji wa kule Mtwara, kwa hiyo siyo tumekaa tunasubiri wateja, tunaendelea kubangua.

“Sido (Shirika la Viwanda Vidogo) ambao ni wabanguaji wadogo, wameshabangua tani sita. Bado kuna viwanda tulikuwa tunaingia navyo mkataba, hadi jana (juzi) tumeingia mikataba minne na bado tutaingia mingine zaidi ya 12,” alisema.

Meneja masoko wa kampuni ya Hawte Investment Ltd ya Mtwara, John Joseph alisema wako katika hatua za mwisho za kuingia mkataba na Serikali wa kubangua korosho.

“Mkataba tunasaini muda si mrefu, mazungumzo yamefika mwishoni kabisa. Ni mambo machache tu wanaweka sawa kisha tunaanza kazi,” alisema Joseph.

Mmoja wa maofisa wa kampuni ya Export Trading ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini alisema bado wanaendelea na mazungumzo na Serikali.

Inaelezwa kuwa kuna jumla ya viwanda 23 vya kubangua korosho na ambavyo uwezo wake uliosimikwa sasa ni kubangua jumla ya tani 42,200. Hata hivyo, uwezo wa mashine kwa kiwanda kimoja ni tani 11,142 kwa mwaka sawa na asilimia 26 tu ya uwezo uliosimikwa wa viwanda hivyo.

Taarifa hiyo ya timu ya pamoja ya wataalamu inaonyesha matarajio ya uvunaji wa korosho kwa msimu wa mwaka 2018/19 kufikia jumla ya tani 275,191 na kama viwanda vinane vinavyofanyakazi vingebangua korosho kwa kiwango kinachotakiwa cha tani 127,200 kwa mwaka, kazi hiyo itafanyika kwa miaka miwili.

Taarifa hiyo pia inaonyesha kuwa kuna viwanda 12 vilivyobinafsishwa vikiwa na uwezo wa kubangua tani 116,000 lakini sasa uwezo huo umeporomoka hadi kufikia tani 16,700 huku viwanda vya sekta binafsi vilivyokuwa na uwezo wa kubangua tani 11,200 vikibangua tani 2,245 na kufanya jumla ya korosho zinazobanguliwa kwa mwaka kwa viwanda vyote kuwa tani 18,945.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya watalaamu, zipo sababu mbalimbali za kushindwa kufikia malengo ya ubanguaji ikiwamo suala la teknolojia, uduni wa viwanda, mtaji mdogo wa wanunuzi wa ndani na kukosa nguvu ya namoja kwenye mnada na kutokutumia bidhaa nyingine zitokanazo na korosho na wingi wa kodi kwa wenye viwanda.



Chanzo: mwananchi.co.tz