Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yawainua Wamachinga

1d5fe9aaef9d6a28ed3ad8f321e87e98 Serikali yawainua Wamachinga

Wed, 3 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imesema kuanzia sasa wafanyabiashara wadogo nchini watatambulika rasmi kama Wamachinga na jina hilo litakuwa nembo ya wafanyabiashara hao.

Pia imewataka Wamachinga wasitumike katika kudhoofisha uchumi wa nchi kwa kusaidia watu wengine kukwepa kodi.

Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye Kongamano la mashauriano kati yake na Wamachinga kutoka mikoa yote nchini lililofanyika jana Dar es Salaam.

Waziri Mkuu alisema kwa kuwa kaulimbiu ya wafanyabiashara hao inasema 'Wamachinga ni fursa sahihi ya kujenga uchumi', hivyo kuanzia sasa serikali imeamua kulirasimisha jina hilo na tangu sasa wafanyabiashara wadogo watajulikana kama Wamachinga.

“Wamachinga ni watu muhimu na mmekuwa suluhisho la mahitaji kwa watu wa uchumi wa juu, kati na chini,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza kuwa kutokana na umuhimu wa kazi zao, aliwataka Wamachinga wasitumike katika kuwasaidia watu wengine kukwepa kodi.

Alisema kama mmachinga analipa kodi ya Sh 20,000 kupitia kitambulisho , hatakiwi kutumiwa na wafanyabiashara wengine wanaowapatia bidhaa zao waziuze kwa kuwa kwa kufanya hivyo wanawasaidia kukwepa kodi.

“Mnapopokea bidhaa za wenye maduka makubwa bila muhusika kukupa risiti za mauzo, unakuwa unamsaidia kukwepa kodi wakati wewe unalipa Sh 20,000 ya kitambulisho, msifanye hivyo,” alisema Majaliwa.

Pia aliwaambia Wamachinga kuwa kufanya migomo maeneo ya kazi zao, kuvamia maeneo muhimu kama vile kupanga bidhaa katikati ya barabara na kupanga bidhaa zao mbele ya maduka ya wafanyabiashara wengine, ni kitendo cha kuwasaidia watu hao wasilipe kodi kwa kuzuia shughuli zingine za kiuchumi zifanyike kwa utulivu.

Pamoja na changamoto hizo, Waziri Mkuu alisema serikali inatambua mchango wa Wamachinga wapatao milioni 3.1 nchini kwa kuwa biashara zao zinachingia asilimia 27 katika Pato la Taifa na pia asilimia 23 ya nguvu kazi iko kwenye sekta ya wafanyabiashara wadogo jambo ambalo limesaidia kutatua changamoto ya ajira.

“Serikali itaendelea kujenga miundombinu bora kwa ajili ya wamachinga kufanya biashara kwa urahisi ikiwemo kuwapatia vitambulisho vya kisasa na kuwapatia maeneo ya kufanya biashara yenye mikusanyiko ya watu,” alisema.

Kuhusu vitambulisho vitakavyotolewa, alisema vitakuwa na alama zote muhimu zinazomtambulisha mmachinga ikiwemo picha ya muhusika, majina halisi, kitaunganishwa na mifumo mingine ya kiserikali ikiwemo NIDA, bima za afya na kitatumika kwa miaka mitatu badala ya mwaka mmoja kabla kukihuisha tena.

Kuhusu kupata mikopo benki, Majaliwa aliwataka Wamachinga kujiunga kwenye vikundi na kusajiliwa kwenye halmashauri zao ili vitambulike rasmi na kuaminika na mabenki katika kupata mikopo.

Aidha, Waziri Mkuu aliwaambia wamachinga kuwa kuanzia sasa watakuwa chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Alisema Wzara ya Tamisemi ndiyo itakuwa na jukumu la kuratibu biashara zao, kuwapatia maeneo ya kufanya biashara pamoja na kuwapatia elimu.

Pia aliwataka wakurugenzi watendaji wa halmashauri zote kwa kushirikiana na uongozi wa Shirikisho la Wamachinga kuwa na takwimu sahihi za wamachinga kwenye maeneo yao na kwa kufanya hivyo kutakuwa na takwimu sahihi kwa nchi nzima.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga nchini, Masanja Matondo, alimweleza Waziri Mkuu mambo sita ambayo wamachinga wanayaomba kwa serikali.

Mambo hayo ni kutaka Wamachinga kutambuliwa na mamlaka za serikali, kupatiwa mikopo na mitaji, kupatiwa ujuzi wa biashara, kuwa na uhusiano mzuri na vyombo vya serikali pamoja na kupatiwa maeneo ya kufanyia biashara.

Matondo pia alimwomba Waziri Mkuu awasaidie wamachinga wa Mkoa wa Mbeya kwa kuwa bado wanasumbuliwa kufanya biashara kwenye baadhi ya maeneo. Pia aliiomba serikali kuwajumuisha akina baba kwenye mikopo inayotolewa na halmashauri kwa akina mama na vijana.

Chanzo: habarileo.co.tz