Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yawabana koo wakandarasi ujenzi miradi ya Maji

WhatsApp Image 2022 09 08 At 11.03.42 AM 1080x640.jpeg Serikali yawabana koo wakandarasi ujenzi miradi ya Maji

Thu, 8 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba ametaka hadi kufikia Septemba 30, 2022 miradi yote ya maji nayotekelezwa kwa fedha za Uviko-19 Mkoani Kagera, iwe imekamilika na ianze kutoa huduma kwa Wananchi.

Kemikimba ametoa maagizo hayo wakati alipotembelea mradi wa maji wa Buyango septemba 7, 2022 kujionea hali ya utekelezaji na kusema miradi hiyo ilitakiwa iwe imekamilika mwezi juni na kuchelewa kwake kunafanya wananchi kuendelea kupata adha ya maji.

Amesema, “Nimejionea hali ya utekelezaji wa mradi huu ambao ulitakiwa kukamilika mwezi juni, ila kutokana na changamoto ambazo tayari tumeshazitatua naagiza miradi yote mkoani Kagera ukiwemo huu ikamilishwe kabla ya tarehe 30 mwezi huu.”

Kemikimba ameongeza kuwa, “Sisi kama wasaidizi wa Rais kwenye sekta ya maji hatutakuwa kikwazo cha wanachi wa Buyango na Kagera kwa ujumla kupata maji safi na salama na yenye kutosheleza.”

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu huyo, ameagiza vituo vya kuchotea maji vilivyokamilika vya mradi wa maji wa Kyaka – Bunazi vikabidhiwe kwa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (BUWASA), ili vitoe huduma ya maji kwa wananchi.

Awali, Mkandarasi wa kampuni ya Advanced Engineering Company Ltd, Athumani Mkono amesema sababu za kuchelewa kwa mradi huo ni kukosekana kwa mabomba, kuwepo kwa miamba kwenye njia za kupitisha mabomba na kuchelewa kwa fedha.

Taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, iliyotolewa na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Missenyi, Mhandisi Andrew Kilembe imesema mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 575.8 uliofikia asilimia 85 ya utekelezaji wake.

Akiongea kwa niamba ya wananchi wa kata ya Buyango, Diwani wa Kata hiyo ambaye pia ni Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Missenyi, Regina Lwamuganga amesema kukamilika kwa mradi huo kutawasaidia wananchi hasa akina mama ambao wamekuwa wakifuata maji umbali wa zaidi ya kilomita tatu.

Miradi hiyo ya maji, ambayo imetembelewa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhadisi Nadhifa Kemikimba ni ule wa Buyango, Byamutemba na vituo vya kuchotea maji vya mradi wa Kyaka – Bunazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live