Serikali nchini, imeombwa kuangalia utaratibu wa usambazaji wa mbolea ya ruzuku, kutokana na usumbufu wanaoupata wakulima kwa kukosekana vituo vya karibu ambavyo vingekuwa msaada kwao.
Ombi hilo limetolewa na baadhi ya wakulima wa baadhi ya Vijiji vya Wilaya ya Babati na kuongeza kuwa, wamekuwa wakitumia gharama kubwa kwa ajili ya usafiri kufuata Mbolea Mjini, na kwamba hawaoni unafuu wa ruzuku iliyotangazwa na Serikali.
Kufuatia madai hayo, Afisa Kilimo Mkoa wa Manyara, Paulina Joseph, amekiri uwepo wa changamoto hiyo na kuahidi kuangalia namna ya kuongeza mawakala maeneo ya karibu na kusema tayari wameweka mawakala wilaya ya Babati, Hanang’, Mbulu, Kiteto na Simanjiro.
Amesema pembejeo zingine kama mbegu zipo karibu kila eneo changamoto ni kwenye mbolea pekee hivyo wakulima waifuate mbolea hiyo inapopatikana ili wasipitwe na msimu wa kilimo wakati serikali inatafuta utatuzi.