Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yavunja rekodi kiuchumi

04300d88e2e39f5007c7a48d7f749a7c Serikali yavunja rekodi kiuchumi

Sat, 8 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imeeleza mafanikio kiuchumi ndani ya miaka mitano ya uongozi wa Awamu ya Tano ambapo imeweka rekodi kwa ukubwa wa Pato la Taifa, udhibiti wa mfumuko wa bei na kiwango kikubwa cha ukuaji uchumi kuliko wakati wowote tangu nchi ipate uhuru.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi aliainisha hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati akielezea kazi iliyofanywa na serikali katika kipindi cha miaka mitano chini ya Rais John Magufuli.

Dk Abbasi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, miongoni mwa vigezo alivyozungumzia ni kukua kwa pato la taifa, pato la mtu mmoja mmoja, ukuaji wa uchumi kwa mwaka na ongezeko la mapato ya serikali ambavyo vyote vimevunja rekodi kwa ukuaji katika serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.

Pato la taifa

Abbasi ambaye alishukuru msingi uliowekwa na awamu zote zilizotangulia, alisema pato limeongezeka kutoka dola za Marekani 622 na kupanda maradufu mpaka dola 1,063 Juni 2019 huku thamani yake ikiwa ni sawa na Sh 2386.

“Lakini pato hilo lililoongezeka la mwananchi, ni kubwa kuliko wakati wowote katika historia ya nchi hii,” alisema na kuonesha takwimu kwenye awamu nyingine akiendelea kushukuru msingi uliowekwa na serikali ya awamu ya kwanza hadi ya nne.

“Awamu ya tano imefanya kazi kwa kasi zaidi kutekeleza misingi iliyoongeza siyo tu pato la taifa bali pia pato la mwananchi mmoja mmoja,” alisema.

Alifafanua kwamba katika awamu ya kwanza, ilikuwa dola 90 ikaenda mpaka dola 205 kwa awamu ya pili ambayo viwango vya ubadilishaji wa wakati huo ilikuwa ni sawa na Sh 46,722. Awamu yatatu, mwaka 1996 mpaka 2005, pato la Mtanzania lilipanda tena kutoka dola 205 hadi 331 ambazo kwa kizio cha wakati huo ilikuwa ni sawa na Sh 277,000 . Katika awamu ya nne, mwaka 2006 hadi 2015, pato lilipanda hadi dola 622 kutoka dola 331 na wakati huo ilikuwa ni sawa na Sh 979.

“Hatimaye sasa katika hii miaka minne, tumetoka dola 622 mpaka dola 1,060 na kitu. Kwa sababu kizio cha kuingia kipato cha kati ni dola 1,036,” alisema Dk Abbasi.

Rekodi tangu uhuru

Akizungumzia kigezo cha kasi ya ukuaji wa uchumi, Dk Abbasi alishukuru Watanzania wanavyoshiriki na kuwezesha katika kipindi cha miaka minne uchumi kukua kwa wastani wa asilimia 6.9 kwa mwaka. Kwa mujibu wa msemaji mkuu wa serikali, kiwango hicho cha asilimia 6.9 ni kikubwa kuliko wakati wowote tangu nchi ipate uhuru.

Alitoa takwimu za kuonesha wastani wa ukuaji uchumi katika awamu zote huku akishukuru serikali zote zilivyoweka msingi uliosaidia serikali ya awamu ya tano kwenda kasi na kuharakisha maendeleo.

Kwa upande wa serikali ya awamu ya kwanza, alitoa mfano kwamba wastani wa ukuaji wa uchumi kwa takwimu zilizopatikana mwaka 1961 hadi 1985, uchumi ulikua wastani wa asilimia 3.1 kwa mwaka.

Katika awamu ya pili, mwaka 1986 hadi mwaka 1995, uchumi ulikua kwa asilimia tatu ukicheza sawa na awamu ya kwanza. Wakati wa awamu ya tatu, 1996-2005 uliongezeka hadi wastani wa asilimia 5.7 ya ukuaji wa uchum.

Alisema wakati wa awamu ya nne, uchumi uliendelea kukua na wastani ukafika asilimia 6.3 . “Kwa miaka minne iliyopita tukielekea mitano, wastani wa ukuaji uchumi umepanda kutoka asilimia 6.3 ya mwaka 2005 hadi 2015 umekwenda asilimia 6.9… Ni ukuaji mkubwa kwa wastani kuliko wakati wowote katika historia ya nchi yetu nah ii pia kwa afrika, Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi,” alisema.

Pato la serikali

Akizungumzia pato la serikali, alisema katika kipindi hiki cha miaka minne pato la serikali kwa mwezi limeongezeka kutoka Sh bilioni 850 hadi kufikia mwaka 2016 likawa Sh trilioni 1.3.

Alisema, “Kuanzia Julai mwaka jana, ukiangalia wastani mpaka Juni mwaka huu, wastani wa mapato ya serikali umepanda kutoka Sh trilioni 1.3 mpaka trilioni 1.5 na katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha uliopita, kati ya Julai na Juni, mwaka huu kuna rekodi mbili zimewekwa; Ya Julai , Desemba mwaka jana ambapo mapato ya mwezi yalikusanywa kwa kiwango kikubwa kuliko wakati wowote katika historia ya nchi hii.

“Tulifika level (kiwango) cha kukusanya kwa mwezi Sh trilioni 1.9 . Lakini pia kwa taarifa yenu ni kwamba kiwango kinachokaribiana na hicho, kimekusanywa tena mwezi Juni mwaka huu pamoja na kuwapo changmoto za ugonjwa wa Covid19.”

Alisema ongezeko hilo ni matokeo ya kubana mianya ya kukwepa kodi, mwamko wa Watanzania kulipa kodi na usimamizi mzuri wa Wizara ya Fedha na Mipango na taasisi zake hususani Mamlaka ya Mapato (TRA).

Pato la mwananchi

Wachumi pia wanajenga hoja kuwa kukua kwa Pato la Taifa (GDP) lazima kuwe na athari katika pato la mtu mmoja mmoja (kwa vipimo vyote yaani GDP per Capita na GNI per Capita).

Katika miaka mitano ya Rais Magufuli, Pato la Mtanzania mmoja limeongezeka kutoka wastani wa Dola za Marekani 622.0 (Sh 979,513) mwaka 2015 hadi Dola 1,063.3 mwaka 2019/2020 (Sh 2,386,000).

Aidha, Pato hilo limekua karibu maradufu ya Pato la mwananchi kwa wastani wa Serikali ya Awamu ya Nne na kuzidi awamu zote za uongozi wa nchi.

Pato la Taifa hupimwa kwa namna mbili kwa maana ya linalotokana na uzalishaji na mapato ya ndani ya nchi (GDP) na linalohusisha mapato ya ndani na ya kutoka kwa Watanzania walioko au waliowekeza nje ya Tanzania (GNI). Kawaida, GDP ndicho kipimo cha ukubwa na afya ya uchumi wa nchi.

Mfumuko wa bei

Kutokana na ukuaji mzuri wa uchumi, mfumuko wa bei umedhibtiwa. Katika miaka minne na miezi 10, Serikali ya Awamu ya Tano imeweka rekodi ya kupunguza mfumuko wa bei kutoka wastani wa asilimia 9.2 mwaka 2015 hadi asilimia 4.3 mwaka 2019/20.

Msemaji wa serikali alisema pamoja na mafanikio hayo, ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha anafanya kazi kwa bidii huku serikali ikiendelea kuweka sera, mipango na mikakati na kusimamia na kulinda misingi ya uchumi nchi iendelee kuwa katika uchumi wa kati.

"Iko misingi ya kimaadili ya kuizingatia pia wakati huu uchumi wetu ukiwa unakua vyema: kwa hiyo tuepuke rushwa; uvivu kazini; tuache tabia za kisebusebu na kiroho papo, yaani mtu unakuwa wa moto-baridi, leo unaponda hiki, kikifanyika unaponda, kisipofanyika unaponda,” alisema.

Alisema upondaji usiokuwa na faidai ni tabia si tu za kibedui bali pia kiguberi zisizo na nafasi nchini. Alisema taifa hili limepata mafanikio lukuki kutokana na uimara wa serikali , kujituma na kuthubutu.

Taarifa kimataifa

Dk Abbasi alibainisha pia taarifa mbalimbali za kimataifa zinazothibitisha uchumi wa Tanzania unavyokua ikiwamo za Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika kuanzia Desemba mwaka jana zikisifu ukuaji wa uchumi. Pia majarida ya kimataifa kama vile Forbes, yamesifu ukuaji wa uchumi unaotokana na utajiri wa raslimali na utalii nchini.

Chanzo: habarileo.co.tz