Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaupa kipaumbele ujenzi bandari Zanzibar

Bandari DSM Ccm Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi

Wed, 5 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema serikali inaendelea na kazi ya kutekeleza dhana ya uchumi wa buluu kwa vitendo kwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa Bandari ya Mkokotoni itakayowaunganisha wananchi kiuchumi na biashara kwa mikoa jirani ya Tanzania Bara.

Akizindua mradi huo wa ujenzi wa Bandari ya Mkokotoni katika Mkoa wa Kaskazini Unguja katika hatua mbalimbali, Dk Mwinyi alisema kuelekea uchumi wa buluu miradi ya ujenzi wa bandari imepewa kipaumbele cha kwanza ili kufikia malengo ya fursa za uwekezaji kiuchumi.

Alitoa mfano kuwa serikali ipo katika mchakato wa ujenzi wa bandari za Wete, Chake Chake pamoja na Bandari ya Kizimkazi na Shumba Mjini ambayo itaongeza huduma za usafirishaji wa huduma mbalimbali ikiwemo mizigo.

Alisema serikali ipo katika kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Bandari ya Mangapwani ambayo upembuzi yakinifu umekamilika pamoja na wawekezaji kuonesha nia ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa.

‘’Nataka niwaambie wananchi kwamba tumejipanga kutekeleza uchumi wa buluu kwa vitendo katika ujenzi wa bandari mbalimbali lakini pia tupo katika hatua za mwisho za ujenzi wa bandari kubwa ya Mangapwani ambayo upembuzi yakinifu umekamilika,” alisema.

Alipongeza Shirika la Bandari la Zanzibar kwa kugharamia mradi wa ujenzi wa Bandari ya Mkokotoni kwa asilimia 100 hatua ambayo alisema inatia moyo kwa taasisi za serikali kuweza kugharamia miradi mikubwa kwa fedha za ndani.

Aliwaahidi wananchi wa Mkoa wa Kaskazini kwamba serikali itaendelea kukamilisha mradi huo na kuwaunganisha wananchi kiuchumi na uwekezaji katika mikoa jirani ya Tanzania Bara.

‘’Tumetenga Sh bilioni 6.4 kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa bandari ya Mkokotoni ambapo tunataka kuona kwamba bandari hii inakamilika katika hatua zote muhimu kwa ajili ya kutoa huduma zote ikiwemo mizigo,’’ alisema.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, Amour Hamil Bakari alisema ujenzi wa bandari hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya kuona kwamba wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja katika Kisiwa cha Tumbatu wanapata bandari itakayosaidia na kuharakisha kuleta maendeleo ya kiuchumi.

Alisema bandari hiyo ya Mkokotoni ni kiungo muhimu kwa wananchi wa mkoa huo ikiwemo Kijiji cha Mkokotoni hadi Kisiwa cha Tumbatu pamoja na mikoa jirani ya Tanzania Bara ikiwemo Tanga.

Kaimu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Lela Mohamed Mussa alisema ujenzi wa miradi ya bandari katika Kisiwa cha Zanzibar ni muhimu.

‘’Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane tumejipanga kutekeleza uchumi wa buluu ambao kwa sehemu kubwa ni ujenzi wa bandari za aina mbalimbali zitakazosaidia wananchi wetu kiuchumi na kuingiza mapato kwa taifa,’’ alisema.

Akizungumza katika sherehe za uzinduzi wa bandari ya Mkokotoni Unguja, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jaffo aliwataka wananchi wa Zanzibar kulinda mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964 ambayo sasa yamelenga zaidi kufanikisha fursa za kibiashara na uwekezaji.

‘’Matunda ya mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964 ndiyo haya...wananchi zitumieni fursa za kiuchumi na biashara kwa ajili ya kupata kipato na kubadilisha maisha yenu kuwa bora,’’ alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live