Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatumia tril 1/- kupaisha uchumi, kuboresha elimu

D4c8ea4e1ad6a3f1109a80aee0d80f2d Serikali yatumia tril 1/- kupaisha uchumi, kuboresha elimu

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imetoa zaidi ya Sh trilioni 1.05 kutekeleza miradi ya reli ya kisasa, mradi wa umeme, mradi wa kusambaza umeme vijijini, mikopo ya elimu ya juu na kugharamia elimu bila malipo katika nusu mwaka wa mwaka wa fedha 2020/2021.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi, aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dodoma jana kuwa makusanyo kutokana na sekta ya madini, yameongezeka kwa asilimia 120 katika miezi sita ya mwaka wa fedha 2020/2021.

Dk Abbasi alisema kuwa taswira ya nchi imeendelea kuheshimika kimataifa kutokana na historia na misimamo ya Rais John Magufuli. Aliyasema hayo wakati akielezea muhtasari wa kazi ambazo zimeanza na zinaendelea kutekelezwa katika miaka mitano ya Rais Magufuli, baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka jana.

Alisema ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaogharimu Sh trilioni 7, katika nusu ya mwaka wa bajeti, Julai hadi Desemba mwaka jana, serikali ilitoa Sh bilioni 274.1 kuugharamia.

“Mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa umeshafikia zaidi ya asilimia 90 kwa kipande cha Dar-Moro chenye urefu wa kilomita 300 huku kipande cha Moro-Makutupora mkoani Singida chenye kilomita 422 kimefikia asilimia 55 na tayari serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa kipande cha tatu cha Mwanza-Isaka chenye urefu wa kilomita 341,”alisema Dk Abbasi na kuongeza kuwa; “Hivi karibuni nitatoa taarifa ya uzinduzi wa safari za treni katika kipande cha Dar hadi Moro na upokeaji wa vichwa vipya vya kisasa vya treni hiyo ya umeme.

Hivyo niseme reli inakwenda vizuri hatujawahi kukwama” alisema. Kuhusu Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere, alisema mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 30, katika nusu mwaka wa fedha kiasi cha Sh bilioni 274.1 kimetolewa.

Alisema kuwa mradi huo utakamilika ndani ya miaka mwili ijayo. “Mpaka sasa serikali itakuwa imeshatoa zaidi ya Sh trilioni 1.3 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambao unagharimu shilingi trilioni 6.5 na kwa sasa inaendelea mchana na usiku kujenga mabwawa madogo ya akiba ya maji, kuandaa ujenzi wa ukuta wenyewe ambapo mwezi Februari wataanza kumwaga zege” alisema.

Dk Abbasi alisema pia kazi nyingine inayoendelea ni ujenzi wa jengo la kuzalisha umeme, ambao ujenzi wake umeanza huku mitambo ya umeme imeanza kutengenezwa nje ya nchi.

Akizungumzia mradi wa usambazaji wa umeme (REA), Dk Abbasi alisema kazi kubwa inaendelea nchini na kuna mafanikio makubwa, ambapo mpaka sasa vijiji 10,018 kati ya 12,317 vimefikiwa.

“Katika nusu mwaka pekee shilingi bilioni 171.9 zimeshatolewa na wakandarasi wanaendelea kwa kasi. Niwahakikishe ifikapo Juni mwaka huu tufikia malengo ya kila kijiji kuwa na umeme na kama kuna nyumba itakosa umeme basi iwe kwa mtu mwenyewe kutokuunganisha bali umeme utakuwapo” alisema.

Kuhusu sekta ya elimu, Dk Abbasi alisema Rais Magufuli anaendelea kutimiza ahadi zake na kwamba kwenye mikopo ya elimu ya juu Sh bilioni 105 zilitolewa kwa awamu ya kwanza ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

“Na wiki hii serikali imeshatoa shilingi bilioni 103 na wanafunzi 145,000 wanaendelea kupata ‘boom’”alisema. Dk Abbasi alisema serikali imeendelea kugharamia elimu ya msingi na kwamba hadi Desemba 31 mwaka jana ikiwa ni nusu ya mwaka wa fedha, Serikali imeshatoa Sh bilioni 124 kugharamia elimu bila malipo.

Akizungumzia sekta ya madini alisema mapato kwenye sekta hiyo yanayotokana na mageuzi ya Rais Magufuli, yanazidi kuongezeka kwa kuwa Julai hadi Desemba mwaka jana, mapato yameongezeka kwa asilimia 120.6 ya lengo la nusu mwaka na kwamba Sh bilioni 317.5 zilikusanywa.

Dk Abbasi alisema Tanzania imeendelea kuwa na heshima katika taswira ya kimataifa, kutokana na historia yetu, lakini zaidi na misimamo thabiti ya Rais Magufuli katika masuala ya kimataifa na matokeo yameonekana.

“Hii imejidhihirisha kutokana na Rais Magufuli kuchaguliwa na Waafrika kote duniani kushika nafasi ya pili katika viongozi 54 wa Afrika kuwa kiongozi bora wa kisiasa wa mwaka barani Afrika (African Political Leader of the Year 2020) kwa mujibu wa Jarida la AFRICA LEADERSHIP MAGAZINE (ALM).

“Kama nchi pia tumeendelea kupokea viongozi mbalimbali wa kimataifa wakiwemo Rais wa Msumbiji, Rais wa Ethiopia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China.

Ziara hizi ni kielelezo cha kuimarika uhusiano na ushirikiano wetu na nchi mbalimbali duniani” alisema na kuongeza; “Napenda kuwajulisha kuwa tuna ugeni mwingine mkubwa mpya hivi karibuni na tutautangaza muda ukifika.

Chanzo: habarileo.co.tz