Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatuma ujumbe Benki ya Dunia

Ca61daf4e0dc6228fa89bd245924b4eb Serikali yatuma ujumbe Benki ya Dunia

Wed, 20 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuahidi kuisaidia Tanzania kukabili athari za kiuchumi zinazotokana na madhara ya janga la Covid-19 na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine.

Dk Mwigulu alisema hayo jana nchini Marekani alipokutana na kuzungumza na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dk Hafez Ghanem.

Viongozi hao walikutana wakati wa mikutano ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), inayoendelea jijini Washington DC.

Dk Mwigulu alisema Tanzania inafanya jitihada ili uchumi wake urudi kwenye hali ya kawaida kwa kutafuta rasilimali fedha na kuzielekeza kwenye sekta zitakazochochea ukuaji wa uchumi ikiwemo kilimo na kuimarisha sekta binafsi.

“Tumepokea taarifa ya namna Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linavyokusudia kufufua uchumi wetu kwa kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na kuisaidia sekta binafsi hususani wajasiriamali wakiwemo wamachinga,” alisema.

Dk Mwigulu alisema Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na wataalamu wa Benki ya Dunia, IMF na Benki ya Maendeleo ya Afrika, watakutana ili kupitia maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ili utekelezaji wa miradi hiyo ianze mwaka mpya wa fedha 2022/2023.

"Tuna maeneo yanayohitaji uangalizi wa karibu yakiwemo ya mfumuko wa bei, kupanda kwa bei za bidhaa ambayo ni muhimu kwa wananchi wetu na yanahitaji serikali ipunguze kodi na fidia ya fedha hizo zinatakiwa zipatikane kutoka kwenye vyanzo vingine, kama tunavyoendelea na mijadala hii," alisema.

Dk Ghanem alipongeza mabadiliko ya kisera na kiuchumi yanayoendelea nchini Tanzania, ambayo anaamini yatasaidia kukuza uchumi wa nchi na wa wananchi wake.

Aliahidi kuwa benki hiyo itaisaidia Tanzania na nchi nyingine za Afrika kukabili athari za Covid-19 na vita ya Ukraine na Urusi iliyosababisha kupanda kwa bei za bidhaa zikiwemo za mafuta na vyakula duniani kote.

Dk Mwigulu yuko nchini Marekani akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mikutano ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF inayokutanisha magavana wa taasisi hiyo, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live