Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatoa ufafanuzi ulipaji wa kodi

Thu, 7 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

BUNGE limeelezwa kuwa masuala ya kodi nchini hutozwa na taasisi za kikodi kulingana na sheria za kodi zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Wizara ya Nishati katika swali la Mbunge wa Shaurimoyo (CCM), Mattar Ali Salum.

Katika swali lake, alisema Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) hununua umeme wa jumla kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), lakini wanaponunua umeme hutozwa kodi ya ongezeko la thamani(VAT) na Mamlaka ya Mapato (TRA).

“Na wanapokwenda kuuza Zanzibar hutozwa tena kodi ya VAT na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), jambo ambalo hupelekea shirika hilo kuwa na madeni makubwa, Je, serikali inalijua hilo?” Alihoji.

Mbunge huyo pia alihoji serikali ina mikakati gani ya kuondoa kero hiyo.

Katika majibu ya wizara hiyo, ilisema masuala ya kikodi hutozwa na taasisi hizo kulingana na sheria na kwamba pamoja na hali hiyo serikali imeendelea kutatua kero mbalimbali za kikodi katika biashara ya umeme kati ya mashirika hayo.

“Kwa vipindi tofauti TRA na ZRB zimekuwa zikifanya mapitio ya kodi hizo ili kuleta manufaa kwa pande zote mbili za Muungano,” ilisema.

Ilieleza kuwa katika hatua ya kupata ufumbuzi wa kudumu katika jambo hilo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) ilifanya marekebisho ya Sheria ya Kodi na Ushuru Mbalimbali ya Mwaka 2019/20 ambapo umeme unaouzwa kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar uliondolewa VAT na kubaki asilimia sifuri.

Ilisema katika hatua nyingine, SMT kupitia Wizara ya Nishati na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati zinasimamia kwa karibu majadiliano yanayoendelea kati ya Tanesco na Zeco kuhusu bei ya kuuziana umeme.

“Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) na Mamlaka ya Udhibiti (ZURA) zinashirikishwa, lengo ni kuhakikisha kuwa biashara ya umeme kati ya Tanesco na Zeco inafanyika kwa ufanisi na kuyanufaisha mashirika hayo yote mawili pamoja na wananchi kwa ujumla,” ilisema.

Wizara hiyo ilisema suala hilo limefikishwa katika ngazi za watendaji wakuu wa serikali zote mbili wakiwamo makatibu wakuu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live