Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatoa ufafanuzi mkataba wa Irena

Biteko Madini (600 X 355) Serikali yatoa ufafanuzi mkataba wa Irena

Tue, 31 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imetaja faida nane ambazo Tanzania itanufaika kwenye mkataba wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (Irena), ikiwamo kupungua kwa uharibifu wa mazingira unaotokana na uzalishaji na matumizi ya nishati isiyo rafiki na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Oktoba 31, 2023 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alipokuwa akiwasilisha azimio la mkataba wa Irena bungeni jijini hapa.

Ametaja faida nyingine ni kuimarika kwa mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji wa nishati ya umeme na kuliwezesha Taifa kuwa na vyanzo mchanganyiko vya umeme unaoendana na mahitaji ya ukuaji wa kiuchumi na kijamii, pia kutatua changamoto ya vyanzo vya umeme visivyo endelevu na uhakika.

Faida nyingine ni nchi kupata taarifa na takwimu sahihi kuhusu masuala ya nishati jadidifu, fursa za uwekezaji katika nishati hiyo zilizopo, kuimarika kwa utaalamu, teknolojia, utafiti na uelewa kuhusu nishati jadidifu kwa watoa maamuzi na wadau mbalimbali wa nishati.

Dk Biteko amesema faida nyingine kuimarika kwa upatikanaji wa nishati ya gharama nafuu na rafiki wa mazingira ambayo ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini.

Aidha, amesema mkataba huo utachochea kasi ya kufikiwa kwa malengo na shabaha ya Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015, maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020 na Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta ya Umeme wa mwaka 2020.

Pia amesema mkataba huo utachochea kutimiza shabaha za lengo namba saba la malengo ya maendeleo endelevu ya umoja wa mataifa ya mwaka 2030, linalozitaka nchi kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati ya uhakika, endelevu, ya kisasa na gharama nafuu kwa wote.

Dk Biteko amesema mkataba huo utaimarisha kasi ya utekelezaji wa mwelekeo wa dunia kwa sasa kuhusu matumizi ya vyanzo vya nishati visivyo na athari kwenye mazingira na kusababisha mabadiliko ya tabianchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live