Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatoa neno uhaba mafuta ya kula

6766c483bd0df6888548eaeee1c1350b Serikali yatoa neno uhaba mafuta ya kula

Wed, 13 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe amesema mafuta ya kula yatapatikana kama kawaida baada ya kumalizika upakuaji wa bidhaa hiyo inayoingizwa kutoka nje ya nchi kupitia Bandari ya Dar es salaam.

Taarifa ya Ofisa , Mawasiliano Serikalini katika wizara hiyo Eliud Rwechungura imeeleza kuwa changamoto ya uhaba wa mafuta ya kula ilitokana na upungufu wa uzalishaji na kutegemea kuyaleta kutoka nje ya nchi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya jana bei ya mafuta ya kula hutegemea soko la bidhaa hiyo kulingana na msimu na mabadiliko ya bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia.

Rwechungura alieleza kuwa, serikali imezipatia leseni kampuni mbili za uagizaji mafuta ya kula ikiwemo ya East Coast Oil and Fats Ltd na Murzah Wilmar East Africa Ltd.

Alisema, kampuni hizo zimekuwa zikiingiza mafuta ya kula nchini ili kukidhi upungufu wa tani za ujazo 365,000 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Rwechungura, mahitaji halisi ya mafuta ya kula nchini ni tani za ujazo 570,000 kwa mwaka lakini kiasi kinachozalishwa ni tani za ujazo 205,000 kwa mwaka.

Alieleza kuwa, meli mbili zimeingia Bandari ya Dar es salaam ikiwemo ya UACC SHMIYA iliyotia nanga bandarini hapo Desemba 10 mwaka jana.

Rwechungura alieleza kuwa, meli hiyo ilipangwa kushusha shehena Januari 11 mwaka huu na iliruhusiwa kuanza kuyashusha mafuta hayo Desemba 30 mwaka jana na kuikamilisha kazi hiyo Januari tatu mwaka huu.

“Kiasi cha mafuta ya kula yenye ujazo wa 21, 800 MT kimepakuliwa katika meli hiyo na sasa kiko tayari kuingia sokoni”ilieleza taarifa ya Rwechungura na kuongeza;

“Aidha, meli nyingine iitwayo MELATI SATU ya shehena ya mafuta ya kula ya ujazo wa 26,450 MT imetia nanga alfajiri ya tarehe 5 Januari, 2021 katika Bandari ya Dar es Salaam na ratiba ya ushushaji wa shehena inaonesha kuwa ni tarehe 19 Januari, 2021 hadi tarehe 22 Januari, 2021”.

Taarifa ya Rwechungura alisema kuwa Wizara ya Viwanda na biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi zinaharakisha ushushaji mafuta ya kula yanayoingia kutoka nje ya nchi kupitia Bandari ya Dar es salaam ili kuharakisha upatikanaji wa mafuta hayo.

Rwechungura pia alieleza kuwa, Wizara ya Viwanda na Biashara imewekeza nguvu katika Mkoa wa Kigoma kwa kuzingatia agizo la Waziri Mkuu kuhusu ushiriki wa taasisi za umma katika uzalishaji mchikichi kwa ajili ya usindikaji wa mafuta ya kula.

Alizitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na Jeshi la Magereza Tanzania, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), na Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).

Chanzo: habarileo.co.tz