Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatoa msimamo soko la tumbaku

TUMBAKU Serikali yatoa msimamo soko la tumbaku

Mon, 8 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wizara ya Kilimo imesema imepiga marufuku wanunuzi wa zao tumbaku kunyanyasa wakulima na kwamba washindane ili mwenye bei kubwa ndiye auziwe zao hilo.

Waziri wa wizara hiyo, Hussein Bashe alisema akiwa Chunya mkoani Mbeya kuwa awali wanunuzi wa tumbaku walikuwa wakinyanyasa wakulima kwa kigezo cha mkataba.

Bashe alisema katika miaka mitatu hadi minne wakulima wa tumbaku Chunya wamepitia kipindi kugumu kwa kukosa soko.

Alisema wanunuzi wa zao hilo walikuwa wanajipangia bei ya kulipa ikiwemo dola ya Marekani 0.5 dola au dola 0.8 kwa kilo kwa kusema tumbaku hiyo ilikuwa ni ziada kwa kuwa hawakuwa na mkataba.

“Mkulima analima, anavuna mwenzi wa tano, tumbaku yake inawekwa stoo, mnunuzi anakuja mwezi wa nane eti ndio anakuja kuinunua tumbaku kwa sababu tu kuna kitu kinaitwa mkataba, huo mkataba hajamletea mbolea, hajamleta chochote”alisema.

Bashe alisema kwa mara ya kwanza wakulima wa tumbaku wilayani Chunya wameuza kilo ya tumbaku kwa dola za Marekani 2.2 katika ushindani na vimeanzishwa vyama vya ushirika vya ziada.

Aliwatuhumu wanunuzi wa mazao ya wakulima kuwa wanawahonga viongozi wa ushirika Sh 15 kwa kila kilo na akaonya viongozi hao hiyo tabia ya kuwanyonya wakulima ife.

“Mazao ni ya wakulima, viongozi wa ushirika wale saba, nane sio mali yao, hawana mamlaka juu ya mazao ya wakulima, wao tumewapa jukumu la kuwasimamia wenzao…mwenye bei kubwa ndiye atanunua tumbaku ya mkulima…tabia ya viongozi wa ushirika kujinufaisha kwa jasho la wakulima imefika mwisho”alisema na kuongeza;

“Muda wa kuwanyanyasa wakulima wa tumbaku umekwisha, tunaenda kwenye mfumo wa uwazi, mwenye bei kubwa na yule anayelipa ndani ya saa 24 ndiye atakayechukua tumbaku ya wakulima wa Tanzania”

Alisema matatizo ya kiwanda cha tumbaku Morogoro kilichofungwa kwa zaidi ya miaka minne yamekwisha na kitaanza kuzalisha mwaka huu na kimepewa leseni ya kununua tumbaku Chunya mkoani Mbeya.

Bashe alisema uzalishaji wa tumbaku Chunya ulishuka hadi kilo milioni tano na haikuwa na kuna mikakati ili mwaka kesho zizalishwe kilo milioni 16.

Alisema mbolea ya kupandia imeshafika bandarini na unaendelea mchakato ili iwafikie wakulima hivyo akahimiza waongeze juhudi kwenye kilimo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live