Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatoa mitungi 800 ya gesi Mkuranga

Mitungi Nya Gesi Bei.png Serikali yatoa mitungi 800 ya gesi Mkuranga

Sat, 16 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuranga. Baadhi ya wanawake wa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wamekabidhiwa mitungi ya gesi 800 kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mitungi hiyo ya gesi imekabidhiwa jana, Ijumaa Desemba 15, 2023 na Mbunge wa Mkuranga (CCM), Abdallah Ulega aliyeshirikiana na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima.

Shughuli hiyo ilikwenda sambamba na kongamano la wanawake viongozi wilayani Mkuranga.

Ulega ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, amesema mitungi hiyo imetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, akisema hatua hiyo inaonyesha kiongozi huyo wa nchi alivyokuwa kinara wa kuhamasisha nishati safi ya kupikia.

Amesema hivi karibuni Rais Samia alipohudhuria Mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28), alieleza mikakati ya kuwaondoa kinamama katika matumizi ya kuni na mkaa, hivyo utoaji wa mitungi hiyo ni miongoni mwa jitihada za kukabiliana na halil hiyo.

"Rais Samia amekuwa mstari wa mbele wa kuwasaidia wanawake nchini kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwemo matumizi ya kuni na mkaa. Tukiwa Dubai, Rais Samia aliiambia Dunia anapambana na kuhakikisha anakuwa kinara katika Afrika, ili kinamama wapate nishati safi ya kupikia.

"Tumpe 'maua yake', najua si jambo la mara moja, lakini dhamira na nia yake ni kuhakikisha tunaanza safari hii, muda si mwingine bali ni sasa hivi, ndio maana ameongeza mitungi 500 awali alitoa 300," amesema Waziri Ulega.

Akikabidhi mitungi hiyo yenye thamani ya Sh72 milioni, kwa wanawake wa Mkuranga, Dk Gwajima amewataka kuitumia vema na kuwaeleza wengine kuhusu umuhimu wa kutumia gesi katika matumizi yao ya kila siku.

"Tunataka watu kuamini katika fikra ya kutoka katika matumizi ya kuni na mkaa badala yake watumie gesi. Nyie (wanawake) mliopo hapa pelekeni ujumbe kwa wengine kwamba Rais Samia amedharimia kuwakomboa wanawake wa vijijini kwa vitendo," amesema Dk Gwajima.

Kuhusu kongamano la wanawake, Dk Gwajima ameupongeza uongozi wa wilaya ya Mkuranga kwa kuandaa jambo hilo, akisema hatua ni njema inapaswa kuigwa na halmashauri nyingine ili kulijengea uwezo kundi hilo.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasir amesema kila Desemba kunafanyika kongamano la wanawake lenye malengo tofauti ikiwa ni pamoja viongozi kutambua umuhimu wa viongozi wanawake.

Akitoa somo la uongozi, Nasir amewataka wanawake kutambua wamezaliwa kuwa viongozi wa kusimamia masuala mbalimbali yakiwemo makubwa na madogo.

Naye Mkuu wa Idara ya Mauzo wa Kampuni ya Oryx Gas, Shabaan Fundi amesema kampuni hiyo haina jambo dogo hasa linapokuja suala la uwezeshaji wa wanawake, wakiamini ukiinua kundi hilo, umelisaidia Taifa.

"Tunawezesha wanawake ili kulinda mazingira kutokana na matumizi ya kuni na mkaa, lakini pia tunamlinda mwanamke katika matumizi sahihi ya nishati safi ya kupikia.Naomba kina baba kuwawezesha kina mama kwenye gesi," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live