Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatoa kauli sakata la Nyama nchini

NYAMA 1 Serikali yatoa kauli sakata la Nyama nchini

Wed, 27 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Tanzania imewatoa hofu Watanzania kuhusu uwepo wa homa ya mgunda badala yake waendelee kula nyama kama kawaida.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Jumatano Julai 27, 2022, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Profesa Hezron Nonga amesema uvumi unaosambaa ili watu wasile nyama unapaswa kupuuzwa kwani homa ya mgunda siyo kitu kigeni kwa Watanzania.

Hata hivyo, Profesa Nonga amesisitiza nyama iliyopikwa au kuchomwa na kuiva kikamilifu kuwa ndiyo inafaa kwa ajili ya tahadhari kwani ugonjwa wa homa ya mgunda upo Tanzania.

Amesema wanyama ndiyo chanzo ugonjwa ni wanyama hasa panya, paka na popo na kwamba mwaka 2021 zaidi ya mbwa 280 walikufa kutokana na ugonjwa.

Serikali hivi karibuni ilitangaza homa ya mgunda baada ya mlipuko uliotokea mkoani Lindi na kusababisha vifo vya watu na wagonjwa.

Mkurugenzi amesema wataalamu wa mifugo na afya wanaendelea kutoa elimu juu ya namna ya kujikinga na ugonjwa huo ambao unaambukizwa kutoka kwa wanyama na wakati mwingine binadamu mwenyewe kuambikiza wanyama.

"Nyama ya Tanzania iko salama, Watanzania wasiogope kula nyama bado tuko salama na hii si mara ya kwanza tena siyo gonjwa jipya nchini kwetu," amesema Profesa.

Kuhusu udhibiti wa ugonjwa, amesema timu ya madaktari ipo mkoani Lindi kwa ajili ya kufuatilia zaidi na kutoa elimu kama inavyotakiwa ikiwemo chanjo kwa wanyama.

"Homa ya mgunda ni moja ya magonjwa na maambukizi yanayotikana kwa wanyama kwenda kwa binadamu au kutoka kwa binadamu kwenda kwa wanyama (zoonosis)," amesema Profesa Nonga.

Kwa upande wake, msajili wa bodi ya nyama, Dk Daniel Mushi amesema dawa pekee ya kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa huo ni kufuata taratibu za uchinjaji na uhifadhi wa nyama kabla ya kufika jikoni.

Dk Mushi amesema wanaendelea na operesheni kabambe ya kukagua mabucha ambayo si rasmi kwa ajili ya kuepusha kuuza nyama iliyo hatari na wameanzia mkoa wa Kilimanjaro ambao ni moja ya mikoa yenye tatizo.

Amezuia ulaji wa nyama isiyoruhusiwa ikiwemo panya na paka wakati wanyama walioruhusiwa wapo wa kutosha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live