Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatoa bil 260/-  ujenzi bomba la mafuta

Af7253cc8c379849dfcf0a2a78390851.jpeg Serikali yatoa bil 260/-  ujenzi bomba la mafuta

Thu, 12 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imetoa Sh bilioni 259.96 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP ) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Bukome, kijiji cha Nyakato, wilayani Chato, mkoa wa Geita.

Aliwataka wananchi wachangamkie fursa zinazotokana na ujenzi wa bomba hilo litakalopita katika mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Alitaja fursa hizo kuwa ni usafirishaji, ulinzi, chakula, vinywaji, huduma ya malazi, mafuta kwa ajili ya magari na mitambo, bidhaa za ujenzi, shughuli za ujenzi, huduma za mawasiliano na ukodishwaji wa mitambo ya ujenzi.

Dk Kalemani alisema Sh bilioni 28 zilitengwa ili kuwalipa wananchi 9,122 waliopitiwa na mradi wa ujenzi wa bomba hilo na tayari Sh milioni 823 zimelipwa kwa wananchi wanaopisha ujenzi wa kambi.

Alisema ujenzi wa bomba hilo utaanza mwezi ujao na bomba hilo litapita katika wilaya 24, kata 134 na vijiji 257 nchini.

Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James Mataragio alisema mradi huo ni sehemu ya miradi 16 ya kielelezo inayotarajiwa kutekelezwa katika mpango wa tatu wa taifa wa maendeleo na kwamba saba kati ya hiyo ipo kwenye sekta ya nishati.

"Serikali inataka kutumia miradi ya nishati ili kuhakikisha tunafika katika uchumi wa kati wa juu kwani uwapo wa gesi na umeme wa kutosha utasaidia kuhakikisha adhima ya nchi ya kufikia maendeleo ya kiuchumi," alisema.

Wakati akizungumza na akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mkungu, wilayani Chato, mkoani Geita na wawakilishi wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Kanda ya Ziwa katika kongamano la fursa za mradi wa EACOP, Dk Kalemani alisema mradi huo unatarajiwa kuzalisha ajira 10,000 rasmi na zisizo rasmi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz