Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatimua wachimbaji wadogo 5,000 mgodini

9882 Pic+mgodi TZWeb

Sun, 24 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. Serikali mkoani Geita imewaondoa wachimbaji wadogo zaidi ya 5,000 waliokuwa wakiendesha shughuli za uchimbaji katika eneo la Mlima wa Chibugwe uliopo kata ya Mgusu wilayani Geita kwa maelezo kuwa eneo hilo ni mali ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).

Mmiliki wa eneo hilo, Ezekiel Magesa amesema Serikali ilitoa siku 30 za kuondoka lakini katika hali ya kushangaza Juni 22, 2018 ofisa madini wa mkoa, Aly Said aliwataka kuondoka ndani ya saa 24.

Akizungumza na MCL Digital, Magesa amesema uamuzi huo aliouita kuwa ni wa uonevu umewasababishia hasara ya zaidi ya Sh500million kutokana na wachimbaji wadogo waliokua wakifanya kazi katika maeneo hayo kuiba mawe, mchanga unaosadikiwa kuwa na dhahabu, petroli na gololi zilizokua kwenye, "makarasha".

 

Magesa amesema anafanya shughuli za uchimbaji katika eneo hilo tangu mwaka 1984 akiwa na miaka 19 lakini anashangazwa na uamuzi wa Serikali wanaoufanya sasa akiwa na miaka 54.

Akizungumzia uamuzi huo Said amesema ulitokana na maagizo ya kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa iliyomtaka kuwaondoa wachimbaji hao baada ya Magesa anayedaiwa kuvamia eneo hilo, kukaidi agizo la kamati hiyo iliyomtaka kuondoka ndani ya siku 30.

Mkuu wa mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema uamuzi huo umetokana na malalamiko ya GGM kuwa eneo lake limevamiwa kwa muda mrefu, baada ya kamati ya ulinzi na usalama kukutana ilibaini Magesa hana leseni ya umiliki wa eneo hilo.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz