Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatia mkono uuzaji petroli za vidumu

Uhaba Wa Mafuta Vidumu Serikali yatia mkono uuzaji petroli za vidumu

Thu, 14 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali itaanza kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wa vijijini ili kuwawezesha kujenga vituo vidogo vya mafuta nchini kuondokana na matumizi ya mafuta yanayouzwa kwenye madumu na chupa ndogo ambayo muda mwingine sio salama kwa vyombo vya moto.

Waziri wa Nishati, January Makamba alieleza hayo jana, wakati akizungumza na wananchi na waendesha bodaboda wa eneo le Guta wilayani Bunda mkoani Mara huku akibainisha kuwa kwa kuanzia, Serikali imetenga Sh2 bilioni kwa ajili ya mchakato huo.

Makamba yupo katika ziara ya siku 21 katika mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kupokea kero na maoni kuhusu shughuli zinazotekelezwa na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo, likiwemo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Katika maelezo yake, Makamba alisema mafuta yanayouzwa kwenye madumu au chupa sio salama kwa watumiaji wa vyombo vya moto ambapo yanasababisha vyombo vya moto kutomudu kwa muda mrefu na wananchi wamekuwa wakiyanunua kwa bei ya juu.

“Tunataka maeneo haya ya vijijini ili yawe na vituo ili kurahisisha huduma hii na mtu akitaka hata lita mbili azipate. Tumeona wananchi wanadhulumika kwa kununua mafuta kwenye chupa au madumu kwa bei juu, ndio maana Serikali itatoa mkopo huu kwa wafanyabiashara ili kujenga vituo vidogo.

Mbali na hilo, Makamba alisema watarekebisha kanuni za ujenzi wa vituo vya mafuta ili kuwepo kwa kanuni mpya ya vituo vya mafuta vya vijijini ili kusogeza huduma hiyo na wananchi kupata mafuta safi yenye uhakika kwa vyombo vya moto, huku akisema utaratibu wa kupata mikopo hiyo utatolewa. Advertisement

Naye Meneja wa Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kanda ya ziwa, George Mhina alisema mfanyabiashara atakayejenga kituo cha mafuta vijijini hatalazimika kuwa na hati ya umiliki wa ardhi, bali kuwa na muhtasari wa kijiji ulioruhusu kujenga kituo cha mafuta.

Kwa mujibu wa Mhina, ujenzi vituo vya mafuta vya miji ni mfanyabiashara anatakiwa kuwa na hati ya umiliki wa ardhi.

“Kwa vituo vya mjini vinakuwa na mita za mraba 600, lakini kwa vijijini hata akiwa na mita za mraba 20 kwa 20. Pia katika ujenzi wa vituo vya mjini paa lake ni gharama lakini kwa vijiji hata wakiweka bati inatosha, pia chini waweke zege rahisi tofauti na mjini inakuwa ngumu,” alisema Mhina.

Alifafanua kuwa masharti ya mchakato huo hayatakuwa magumu kama vile wanaojenga vituo vya mjini, akisema ada ya leseni itakuwa Sh 100,000 kwa miaka mitano. Pia Mhina alisema walifanya tathimini kwamba ujenzi wa vituo vya mjini gharama yake Sh 200milioni, lakini ukiwa na Sh 40 milioni kwa kuanzia unaweza ukajenga kituo kijijini chenye pampu mbili.

Mwendesha boda wa Guta, Jeremiah Robert alisema hatua ya Serikali kutoa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa vituo itasaidia kupata mafuta ya uhakika na vyombo vyao vya moto, ikiwemo pikipiki na bajaji zitakuwa gharama.

“Muda mwingine mashine zetu za bodaboda zinaharibika kutokana na mafuta ya kununua ya videbe au pikipiki haiwaki. Pia tunanunua kwa bei ya juu, mfano Bunda Mjini wanauza lita moja Sh 3,380 lakini hapa Guta yanauzwa Sh 3,700,” alisema Robert.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live