Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatetea kununua mafuta kwa pamoja

Bei Ya Mafuta Kushuka (600 X 337) Serikali yatetea kununua mafuta kwa pamoja

Wed, 4 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati bei mpya ya mafuta kwa mwezi huu ikitangazwa jana, Serikali imesema ili kuendeleza uhakika wa usambazaji wa nishati hiyo, itadumisha mfumo wa ununuzi wa pamwoja (BPS).

Mwezi uliopita, bei ya mafuta ilivunja rekodi kwa kufika zaidi ya Sh3,000 katika baadhi ya mikoa na huenda hali ikawa mbaya zaidi kuanzia kesho kwa kuzingatia kuwa yatakayouzwa ni yaliyonunuliwa Machi, bei ilipokuwa juu zaidi katika soko la dunia pipa moja likiuzwa kwa zaidi ya dola 120 za Marekani.

Duniani kote bei na upatikanaji wa nishati hiyo muhimu ya kuendesha shughuli za uchumi ni pasua kichwa lakini nchini changamoto ni kupanda kwa bei kwani upatikanaji ni wa uhakika kutokana uagizaji wa pamoja unaofanywa.

Hata hivyo, hivi karibuni baadhi ya wabunge waliibua hoja kutaka kuwe na mfumo huria wakisema utashusha bei ya nishati hiyo, ushauri uliopokelewa na Waziri wa Nishati, January Makamba.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, katika mdahalo wa kipindi cha kipima joto kinachorushwa na ITV, Kamishna wa Petroli na Gesi wa Wizara ya Nishati, Michael Mjinja alisema kama sio BPS kipindi hiki cha vita vya Russia na Ukraine kungekuwa na shida ya upatikanaji wa mafuta nchini kama ilivyo katika baadhi ya mataifa mengine.

“Bei za mafuta bado zinapanda na huenda utulivu usiwepo hivi karibuni lakini upatikaji ni wa uhakika, mafuta yaliyopo yanatosha na yataendelea kuwepo kadri ilivyopangwa,” alisema Mjinja.

Kabla ya kuanzishwa kwa BPS, kamishna huyo alisema Tanzania ilikuwa inashuhudia kukosekana kwa mafuta kwa kuwa kila mtu alikuwa anaagiza atakavyo kwa wakati anaoona unafaa.

“Gharama za kuleta mafuta zikikuwa juu, mzigo ulikuwa unaletwa na meli ndogondogo hivyo zilikuwa zinajazana bandarini na zilikuwa zinatumia muda mwingi kushusha hadi siku 40 jambo ambalo lilikuwa halitoi uhakika wa upatikanaji wa nishati hiyo,” alisema Mjinja.

Meneja Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Kemilembe Kajanabo alisema zabuni za kuingiza mafuta hutangazwa kwa uwazi na mshindi ni anayotoa bei ya chini.

“Kuna kampuni 23 ambazo hushiriki zabuni hiyo, kati ya hizo, saba zimesajiliwa nchini. Kwa mwaka 2021, kati ya kampuni hizo 13 zilishinda zabuni ya kuleta mafuta nchini na kwa kuwa ni wengi sio rahisi hata kupanga njama ya kibiashara kupandisha bei ya mafuta,” alisema Kajanabo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live