Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatangaza msimu wa ununuzi wa Pamba

HASUNGA IPPMEDIA.webp Serikali yatangaza msimu wa ununuzi wa Pamba

Mon, 8 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imetangaza kwamba msimu wa ununuzi wa pamba wa mwaka 2020/2021 utazinduliwa tarehe 15 Juni 2020.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 7 Juni 2020 wakati akizungumza kwenye mkutano maalumu wa wadau wa tasnia ya Pamba uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Benki kuu Jijini Mwanza.

Mhe Hasunga amebainisha kuwa msimu wa Pamba utazinduliwa wakati ambapo serikali imejiweka kando kutopanga bei elekezi katika zao hilo pamoja na mazao mengine badala yake bei za mazao zitatokana na soko.

Amesema kuwa kazi ya serikali ni kuhakikisha kuwa inasimamia uzalishaji bora wa mazao kadhalika kusimamia upatikanaji wa masoko ya mazao ili kuwa na bei nzuri yenye manufaa kwa wakulima.

Amesema kuwa kutokana na usimamizi madhubuti wa serikali kupitia Wizara ya Kilimo, uzalishaji wa pamba umeongezeka kutoka tani 122,178 msimu wa ununuzi wa 2015/2016 hadi tani 348,910 msimu wa 2019/2020.

Waziri Hasunga ameeleza kuwa zao la pamba ni mhimili wa uchumi wa wananchi wengi katika mikoa 17 na Wilaya 56 zinazozalisha zao hilo.

Kiwango kikubwa cha uzalishaji kwa miaka ya karibuni kilifikiwa katika msimu wa ununuzi wa 2011/12 ambapo kiasi cha tani 357,133 za pamba zilizalishwa. Kutokea hapo, uzalishaji umekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka ambapo katika msimu wa kilimo wa 2015/16 uzalishaji ulikuwa tani 122,178 kiasi ambacho ni kidogo kuwahi kuzalishwa nchini.

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipoingia madarakani, hatua kadhaa za makusudi zimechukuliwa na Wizara ya Kilimo ili kulinusuru zao la pamba ambapo malengo ya Wizara kwa sasa ni kuzalisha tani 1,000,000 za pamba ifikapo mwaka 2022/2023.

Amezitaja Hatua zilizochukuliwa na serikali kuwa ni pamoja na kuhamisha makao makuu ya Bodi ya Pamba kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza ili kuwa karibu na maeneo yanayolima pamba na kuwahudumia wakulima kwa karibu zaidi. Kutokana na hatua hiyo, ufanisi wa utendaji na huduma kwa wakulima umeongezeka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live