Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatangaza msimu mauzo ya ufuta 2022/23

Ufuta Biashara Msimu Serikali yatangaza msimu mauzo ya ufuta 2022/23

Thu, 9 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Msimu wa uuzaji wa ufuta kwa mwaka 2022/23 unatarajiwa kuzinduliwa rasmi leo mkoani Mtwara ambapo bei ya mnada ni Sh 2,800 katika zao hilo.

Akitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Marco Gaguti alisema matayarisho yote yameshakamilika.

Alisema Vyama Vikuu vya Ushirika vyote mkoani humo ikiwemo Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba Newala Cooperative Union (TANECU) na Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi Mtwara Cooperative Union (MAMCU LTD) vimeanza ukusanyaji wa zao hilo katika maghala yao tangu Mei 30, mwaka huu.

Alisema mnada wa kwanza unatarajiwa kuwa Juni 10 (kesho) na wakulima wameombwa kupeleka mazao yao ya ufuta katika maghala yaliyoainishwa na vyama vikuu.

''Tumeanza kuona mwenendo wa bei ya ufuta katika maeneo mbalimbali ambayo umeshafanyika mnada, bei ni nzuri na inapindukia shilingi 2,800 kwa hiyo tunategemea bei itaendelea kupanda,” alisema.

Aliwataka wanunuzi wa zao hilo kufuata taratibu zote za kisheria ikiwamo kujisajili kwa ajili ya kuwa wadau kwenye msimu huo.

Matarajio ya mkoa ni kufanya vizuri kwa kupata wastani wa tani 20,000 kwa mwaka huu kutoka tani 11,900 msimu uliopita.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live