Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatangaza fursa mpya mifuko ya plastiki

60486 PLASTIKI+PIC

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imetangaza fursa mpya kwa watu ambao watakuwa bado wanamiliki shehena ya mifuko ya plastiki ifikapo kesho.

Aprili 9, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza marufuku ya matumizi ya mifuko hiyo bungeni jijini Dodoma kuwa ikifika Juni Mosi mifuko hiyo haitakiwi kutumika nchini.

Katika kuitikia katazo hilo la Serikali, tayari mikoa mbalimbali nchini ukiwamo wa Dar es Salaam imeanza kutenga maeneo yatakayotumika kukusanya mifuko kutoka kwa wananchi na wafanyabiashara watakaoisalimisha kuanzia ngazi ya mtaa hadi kata.

Hata hivyo, akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mazingira, January Makamba alisema mifuko itakayokusanywa haitachomwa moto na badala yake, itageuzwa kuwa malighafi ya kutengenezea bidhaa kuu mbili za mabomba na madawati huku akibainisha kuwa kampuni tatu ikiwamo ya Falcon zimejitokeza kufanya shughuli hiyo.

Makamba alitoa kauli hiyo wakati akifunga semina ya wahariri na waandishi wa habari iliyofanyika katika makao makuu ya ofisi za Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Dar es Salaam.

Kabla ya kueleza hatua hiyo, Makamba alisema shughuli ya utekelezaji wa katazo hilo inakwenda vizuri katika maeneo mbalimbali huku akiwashukuru wananchi kwa ushirikiano na mwamko wanaoendelea kuuonyesha.

Habari zinazohusiana na hii

Baada ya kueleza hayo, Makamba alisema kampuni hizo zitatumia mifuko hiyo itakayokusanywa katika maeneo mbalimbali kutengeneza mabomba na madawati huku akisema mifuko ya plastiki itakayokusanywa haitakuwa uchafu bali ni malighafi.

“Hizo kampuni zinazalisha bidhaa hizo kwa kutumika malighafi kutoka nje, lakini kwa kipindi hiki, wataichukua mifuko hiyo na kuirejesha kwa kuifanya iwe kwenye mfumo wa mchelemchele unaotumika kutengenezea bidhaa hizi.

“Yamepatikana makampuni matatu yatakayotumia mifuko yote ya plastiki itakayokusanywa kutengeneza mabomba na madawati. Moja ya kampuni hizo ni hii tunayoikagua Falcon ya Mwanza. Kama una shehena kubwa unaweza kufanya biashara ya kupeleka huko moja kwa moja kabla ya Juni Mosi.” alisema Makamba.

Alisema operesheni ya kuondoa mifuko ya plastiki siyo kazi rahisi kwa sababu mifuko hiyo imeingia kwenye maisha ya watu na imeleta mabadiliko miongoni mwao.

“Zamani tulikuwa tukienda kununua mahitaji tunakwenda na mifuko, lakini sasa haulazimika kwenda nayo kwa sababu unapewa bure unakochukua mahitaji yako,” alisema .

Alisisitiza kuwa suala hilo ni jambo gumu kwa sababu linahusu uchumi na kutakuwa na kampeni mbalimbali zitakazoonyesha Serikali imeshindwa shughuli hiyo na akawataka Watanzania kutoingia kwenye mtego huo.

Katika hatua nyingine, Nemc, imesambaza watendaji wake nchi nzima kwa ajili ya kufanya kazi ya kusimamia utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki.

Meneja wa udhibiti na utekelezaji wa sheria, Dk Madoshi Makene alisema kwa Mkoa wa Dar es Salaam yenye kata 97 kila kata itakuwa na maofisa wa Nemc wawili watakaoshirikiana na watendaji kata kwa ajili ya kusimamia vyema utekelezaji wa sheria na kanuni za katazo hilo.

“Tumeweka watendaji wawili katika mikoa yote isipokuwa Dar es Salaam. Maofisa hawa watavaa majaketi maalumu ili watambulike kwa urahisi,” alisema Dk Makene.

Mbali na hilo, Dk Makene alisema kutakuwa na magari maalumu yatakayopita kwenye maeneo mbalimbali na kutoa matangazo kuhusu katazo hilo na hatua iliyofikia ni lazima shughuli hiyo itafanikiwa.

Akizungumzia kuhusu kanuni za katazo hilo, mwanasheria wa Nemc, Manchare Heche aliwataka Watanzania kushirikiana na Serikali katika mchakato huo, huku akiwaonya dhidhi ya utupaji ovyo wa vifungashio vya plastiki vilivyoruhusiwa.

“Endapo mtu akiwa ana kula korosho au mkate yupo katika gari kisha akakitupa kile kifungashio atapigwa faini ya Sh 20,000 hii ni kwa mujibu ya kanuni ya mazingira.Tuwakumbusha watii maana adhabu hizi zilikuwapo toka zamani.

“Kanuni ya 45(1)ya usimamizo wa taka ngumu, inaeleza yule atakayetupa uchafu wowote atapewa adhabu isipoungua Sh.200,O00 kama mtu binafsi .Kama kampuni ni Sh 5milioni .

Aliwataka wamiliki wa mabasi, kuwaeleza abiria wao wasitupe taka ovyo hasa vile vifungashio vya bidhaa mbalimbali ikiwemo korosho wanapomaliza kuvitumia badala yake waviweka katika utaratibu bora, ambao hautaathiri mazingira.

Pia, mwanasheria huyo alisema mifuko inayotumika kuwekea sabuni ya unga katika maduka mbalimbali na kuuzwa kuanzia Sh 300 na kuendelea haitakiwi kutumika kuanzia Juni Mosi.

Chanzo: mwananchi.co.tz