Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatangaza bei ya sukari mfungo wa Ramadhani

Hii Hapa Bei Elekezi Ya Sukari Serikali yatangaza bei ya sukari mfungo wa Ramadhani

Tue, 12 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati waumini wa dini ya kiislamu wanatarajia kuanza mfungo wa mwezi wa Ramadhani, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza bei elekezi ya sukari ili kuwapunguzia gharama wananchi.

Akitoa taarifa wilayani Mjini Unguja, Waziri wa Wizara Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban ametaja bei ni Sh. 2,650 kwa kilo moja kwa upande wa Unguja na Sh. 2,700 kwa kilo kwa upande wa Pemba.

Amesema hatua hiyo imekuja kufuatia agizo la Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi alilolitoa hivi karibuni katika ziara yake ya kutembelea wafanyabiashara na kusikiliza changamoto zao.

Katika ziara hiyo Dk. Mwinyi ameitaka Wizara ya Biashara kutoa bei elekezi ya kuuzia sukari baada ya serikali kuondoa gharama za kodi katika bidhaa hiyo, ili kupunguza makali ya maisha hasa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Amesema kufuatia agizo hilo Wizara ya Biashara imeelekeza wafanyabiashara wote kushusha bei ya sukari katika kipindi cha Ramadhani na kuuza kwa hiyo iliyotajwa.

Akizungumzia bei elekezi kwa wauzaji wa jumla amesema bidhaa hiyo itauzwa kwa shilingi 123,000 upande wa Unguja na Shilingi 126,000 kwa upande wa Pemba ambapo waingizaji wa bidhaa hizo watauza kwa shilingi 121,000 kwa upande wa Unguja na shilingi 124,000 kwa upande wa Pemba kwa ujazo wa kilo 50.

Amesema kuwa bei hizo zimezingatia utoaji wa kodi na faida kwa kila mmoja hivyo aliwataka wafanyabiashara hao kutekeleza agizo hilo, kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yoyote atakaekwenda kinyume na agizo hilo ikiwemo kufutiwa leseni ya biashara.

Aidha, amewataka watendaji wa Tume ya Ushindani Halali ya Biashara kutekeleza wajibu wao na kuhakikisha sukari inauzwa kwa bei elekezi katika kipindi chote cha mwezi mtukufu wa Ramadhan mpaka itakapotangazwa bei nyingine.

Pia, amewataka wafanyabiashara kutopandisha bei kwa bidhaa ambazo hazijatolewa bei elekezi na kuweka unafuu kwa wananchi ili kumudu gharama za mwezi huo.

"Hiki si kipindi cha kuchuma faida nyingi za kifedha ni kipindi cha kuchuma thawabu, hivyo tuwe na mazingatio na tukumbuke kwamba tunatoa unafuu kwa wananchi wenzetu," amesema.

Kadhalika amewataka wakuu wa mikoa, wilaya na masheha kuisaidia Serikali katika kuhakikisha dhamira ya Rais Dk. Mwinyi ya kuwasaidia wananchi katika kipindi cha Ramadhani na kuhakikisha wanapata mahitaji yao kwa bei nafuu inafikiwa.

Kabla ya Serikali kutangaza bei elekezi sukari ilikuwa inauzwa Sh. 3,000 kwa kilo moja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live