Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yataka nafuu bei ya saruji

A652bdf6f36c1efa9a179bc647e91b41 Bei ya saruji imekua ikipanda kila kukicha

Thu, 12 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ametoa rai kwa kampuni zinazozalisha saruji nchini ziangalie gharama zao za uzalishaji ili kuleta nafuu kwa wananchi na serikali inayohitaji bidhaa hiyo kwa wingi katika kutekeleza miradi ya kimkakati.

Dk Mwigulu alisema hayo alipokutana na kuzungumza na viongozi wa Kampuni ya Afrisam ambayo ni mmoja wa wanahisa wa Kiwanda cha Saruji cha Tanga.

Aliishukuru kampuni hiyo kwa kufanikisha upatikanaji wa saruji kwa wakati katika utekelezaji wa Mradi wa Sh trilioni 1.3 za kukabili athari za janga la Covid-19.

Aliwaomba wazalishaji hao wafanye hivyo wakati huu bei za vitu ikiwa imepanda kutokana na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine.

Alikumbusha namna Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ilivyokaa na wawekezaji hao wakati wa kujenga madarasa na kuwaomba wasipandishe bei kwa sababu ya uhitaji wa bidhaa hiyo uliokuwa umesababishwa na mahitaji ya ujenzi wa madarasa na walikubali kufanya hivyo bila kuongeza gharama zaidi.

Dk Mwigulu alikumbushia pia hivi karibuni wakati bei za vifaa vya ujenzi zilipopanda, waliitikia tena wito wa serikali wa kuwaomba waendelee kuangalia bei ya saruji na kusimamia gharama za uzalishaji.

“Rai yetu, haya mambo ya bei kuongezeka yanaendelea hasa baada ya kuja hili jambo jipya la vita vya Urusi na Ukraine, tuendelee kukabiliana na majanga ya namna hii huku tukiwajali wananchi masikini, sisi huku kwenye sekta ya uzalishaji tukichoka kubeba mzigo, wananchi wetu ambao ni watumiaji wa mwisho watachoka zaidi,” alisema Dk Mwigulu.

Aliwahakikishia wawekezaji hao kwamba serikali itawalinda na kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya biashara kwa kuwa ni msisitizo uliotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Alisema ili kuwezesha uwekezaji mkubwa uendelee kuja Tanzania ni muhimu kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kwa ajili ya kuzalisha ajira na pia vyanzo vipya vya kodi ambavyo vitawapunguzia mzigo na kuwapatia fedha wananchi kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo.

Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya AfriSam, Erick Diack alisema kampuni yake ipo nchini tangu mwaka 1996 na imewekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 190.2 (Sh bilioni 55.7) kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2016.

Diack alisema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.2 kwa mwaka na katika kipindi kifupi kijacho wanakusudia kuongeza uwekezaji na ufanisi kwa kufunga mitambo mingine yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live