Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yatahadharisha uwekezaji hisa za Airtel

Thu, 1 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Serikali imesema haiutambui mpango uliotangazwa na kampuni ya Bhart Airtel kukaribisha wanahisa wapya kwa kuuza hisa zake za awali (IPO) katika Soko la Hisa London (LSE), Uingereza.

Wiki iliyopita, kampuni hiyo ilitoa taarifa yake kuhusu kuwakaribisha wawekezaji wa kimataifa walionunua hisa za Dola 1.25 bilioni za Kimarekani katika mpango wa Airtel Africa kutafuta Dola 4.4 bilioni zitakazosaidia kuimarisha operesheni zake kwenye nchi 14 za Afrika pamoja na kulipa deni lake linalofika Dola 5 bilioni.     

Akizungumza na wanahabari leo, Oktoba 31, Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka amesema kilichofanywa na kampuni hiyo ni batili nchini.

"Tunaamini kampuni ya Bharti Airtel itafuata utaratibu wa kumshirkisha mbia mwenza ambaye ni Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika mchakato mzima wa kuwakaribisha wanahisa wapya," amesema Mbuttuka.

Bharti Airtel kampuni kubwa ya mawasiliano inayoshika nafasi ya sita duniani yenye makao makuu nchini India, ndiye mmiliki wa Airtel Tanzania inayotoa huduma nchini.

Kwa siku za karibuni, Airtel Tanzania imekuwa na mgogoro wa umiliki wa hisa zake kati ya wabia wawili wakubwa, Tanzania na Bharti Airtel.

Mbuttuka amesema kwa kuwa Airtel Tanzania inamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na Bharti Airtel, uamuzi wowote wa uuzaji na uhamishaji hisa au ukaribishaji wa wanahisa wapya unapaswa kuishirkisha Serikali.

Bado Serikali na Airtel Tanzania zinaendelea na mazungumzo kupata muafaka wa umiliki wa kampuni hiyo pamoja na uendeshaji wake.

Katika hatua za awali za kukamilisha IPO inayotarajiwa kufanyika Septemba mwakani, tayari Airtel Africa immewapata wawekezaji sita wa kimataifa wakiwamo Warburg Pincus, Temasek, Singtel, Soft bank Group International na wengine.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz