Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yasisitiza tumekidhi vigezo uchumi wa kati

Ab5472af692917c5f6e938e50e35a7aa Serikali yasisitiza tumekidhi vigezo uchumi wa kati

Sun, 14 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imebainisha kuwa Tanzania imeingia uchumi wa kati baada ya kutimiza vigezo vyote vinavyotakiwa na kamwe haikutuma maombi wala kulipa fedha kuingizwa kwenye nafasi hiyo.

Pia, imeelezea sababu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutumia vikosi vya mkakati kukusanya mapato kuwa ni baada ya wadaiwa kubainika kufanya ujanja na kutumia mbinu kukwepa kodi jambo linalokubalika kisheria kuundiwa vikosi mkakati na kufuatiliwa.

Hayo yalielezwa bungeni Dodoma jana na Waziri wa Katiba na Sheria Dk Mwigulu Nchemba wakati akihitimisha hoja ya Mipango ya Maendeleo ya Kitaifa ya muda mfupi na mrefu iliyowasilishwa bungeni hapo mwanzoni mwa wiki hii.

Mipango iliyowasilishwa ni pamoja na Mpango wa Kitaifa na Mwongozo wa Bajeti kwa mwaka 2021/22 na Mpango wa Maendeleo wa Tatu wa Miaka Mitano wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26.

Alisema katika majadiliano ya wabunge bungeni humo kuna baadhi yao walitoa hoja kana kwamba kipato kilichopimwa ni kidogo na kutilia mashaka dhana yenyewe ya kwamba Tanzania ni uchumi wa kati.

“Kwanza utaratibu wa kuingia uchumi wa kati ni utaratibu ambao unazingatia vigezo. Tanzania kuingia uchumi wa kati haikutuma maombi ya kwamba tunaomba na sisi tuingie kwenye nchi ya kipato cha kati. Hatukufanya application na wala Tanzania kuingia kipato cha kati haikulipiwa. Ni tofauti na utafiti unaweza ukai-comission team fanyeni utafiti huu mniletee ripoti," alisema Mwigulu.

Alibainisha kuwa nchi kuingia kwenye uchumi wa kati ni lazima itimize vigezo vinavyozingatiwa na taasisi kubwa zinazoheshimika duniani ambazo ni Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na wachumi wote walioitangaza nchi kwamba ni ya uchumi wa kati.

“Wala sio mashabiki wa CCM, ni taasisi za wasomi waliobobea na hawajaanza kwa kuitangaza Tanzania, ziko nchi ambazo ziliwahi kufika kule na zimefika kule kwa kuzingatia vigezo na vigezo vyenyewe hata hapa sisi ukianza kuangalia tangu tumeanza kutekeleza mpango tumevifikia," alisema.

Dk Nchemba alisema kwa yule ambaye ataifanyia tathimini Tanzania kuhusu kuingia kwake katika kundi la uchumi wa kati kiungwana lazima atafikia katika majawabu kwamba inakidhi vigezo.

“Tulitarajiwa tufike huko mwaka 2025, tumefika mapema kabla ya muda ule kwa sababu ya ujasiri na uthabiti wa Rais wetu (John Magufuli) kwa sababu kuna mambo ambayo yameenda kwa kasi kubwa na kwa kiasi kikubwa kuliko ambavyo imetekelezwa kwa muda mrefu," alieleza.

Alitolea mfano vigezo vilivyoiingiza nchi hiyo katika kundi hilo kuwa ni kupimwa pato la mtu mmoja mmoja ambalo limefikia wastani wa dola za Marekani 1,036, kupungua kwa utegemezi wa bajeti na kuongeza fedha kwenye matumizi ya huduma za kijamii.

Vigezo vingine ni kuboreshwa kwa miundombinu katika nchi husika. "Ukienda kwenye wastani ambao waliutumia na wakaja na majawabu yale, utaona wastani wa pato la mtu mmoja mmoja, income per capital uliongezeka kutoka shilingi milioni 1.9 kwa mwaka 2015 hadi kufikia Sh milioni 2.5 kwa mwaka 2019.”

Alisema tayari nchi ilishavuka lengo la kigezo ikiwemo eneo la kupungua kwa utegemezi kibajeti." Angalieni ninyi wenyewe utegemezi wa bajeti ulivyopungua mwaka 2015/16 bajeti yetu tuliyokuwa nayo ilikuwa takribani Sh trilioni 22. “Hivi tunavyoongea tumeshavuka Sh trilioni 34 na utegemezi umepungua zaidi.”

Waziri Nchemba alisema vigezo vingine katika eneo la afya katika miaka mitano serikali ilitumia zaidi ya Sh trilioni tatu katika kuboresha sekta ya afya, miundombinu ilitumia zaidi ya Sh trilioni 8.6, utawala bora Sh trilioni moja na usafiri wa majini Sh trilioni moja.

“Wewe unayepinga kwa nini unaona sifa kuitwa masikini? Yaani wenzako wameshakuangalia wakaona wewe umeshaondoka kwenye umasikini, whether unajisikia bora zaidi wakuone wewe ni masikini, angalia nchi inayoweza kutoa shilingi bilioni 24 kila mwezi kupeleka elimu kwa watoto wake na haijakwama inatoa bilioni 700 kulipia watoto kwenye elimu ya juu, tunaita mikopo," alisema.

Alisema kimsingi fedha zote hizo za elimu ni bajeti ya serikali kwa sababu haikopi benki bali ni bajeti ya serikali na kuongeza kuwa wale aliowaita wapiga ramli wanaombeza Rais Magufuli, watambue kuwa nchi inasonga mbele hairudi nyuma na inakwenda kanani.

Kuhusu suala la vikosi vya mkakati kukusanya mapato, Dk Nchemba aliwaomba wabunge wanapozungumzia suala hilo la makusanyo wachukue tahadhari.

“Tuna kipindi tumekipita ambacho kulipa kodi, elimu ya mlipa kodi, uhiari na uzalendo ilikuwa jambo kubwa na gumu sana kwa watu wetu walio wengi hasa wafanyabiashara wakubwa na walipa kodi wakubwa ukwepaji wa kodi ulikuwa mkubwa,” alisema.

Aliwataka wabunge kufuatilia taarifa za vikao vya Bunge na watabaini namna ambavyo kilio cha ukwepaji kodi kilivyokuwa kikubwa hasa kwa wafanyabiashara wakubwa kiasi cha kufanya walipa kodi zaidi wa Tanzania wawe ni watumishi wa umma.

“Na kulikuwepo na serikali bubu, serikali ikipanga namna ya kukusanya kodi, kulikuwepo na reaction ya serikali moja bubu ipo kule tu yenyewe mkipanga bajeti ina hire ndege na kuja wakisema bajeti hii haitatekelezeka," alieleza.

Alisema kupitia ujasiri wa Rais pamoja na ubunifu wa Waziri na timu yake ya wataalamu ikiwemo TRA wamepiga hatua kubwa katika eneo hilo.

Alisema mpaka sasa ana uhakika kwamba TRA haijaacha jukumu lake la kukusanya mapato lakini inapokuja suala la kutumia vikosi vya mkakati hutokana na uwepo wa taarifa kwamba mlipakodi husika ana viashiria vya kutokulipa kodi ipasavyo.

Alisema baada ya hapo timu hutumwa kwenda kukagua, ambayo ni mamlaka ya mapato na wataalamu wao na ikitokea mlipakodi hataki kulipa, ama inatokea amekata rufaa na na uamuzi ukitoka kwamba anatakiwa alipe ama inatokea kuna taarifa zinazoonesha kuna ukwepaji mkubwa. Hapo ndipo timu maalumu inapelekwa kufuatilia.

Alisema Kamishna wa Mamlaka ya Mapato kwa kutumia sheria inayomruhusu kutengeneza kikosi kazi kama ambavyo Sura ya 348 ya Sheria ya Utawala wa Kodi inampa mamlaka Kamishna kuunda vikosi na kushirikisha taasisi zingine za umma, kifungu namba 64 na vifungu vidogo mpaka 67, kwenda kusaidia.

“Wale waliozoea kukwepa kodi, kuwaachia mzigo wale watu wengine na kupata mapato hayo ambayo yalitakiwa yakasaidie huduma za jamii wanayageuza yawe ya kwao, niwahakikishie mazingira ya wao kufanya ukwepaji wa aina hiyo, mambo yataendelea kuwa magumu tu," alisisitiza.

Chanzo: habarileo.co.tz