Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yasisitiza hakuna shida katika Deni la Taifa

Tutubalikf.jpeg Mlipaji Mkuu wa serikali awatoa hofu Watanzania

Tue, 15 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu Wwizara ya Fedha, Emmanuel Tutuba, amesema deni la taifa ni himilivu na serikali inakopesheka, hivyo hakuna sababu za Watanzania kua na wasiwasi.

Vilevile, amesema ili kujiimarisha vizuri kiuchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walikubaliana kujiwekea utaratibu wa kuweka akiba ya fedha za kigeni isiyopungua miezi minne, zinazokidhi kuagiza bidhaa toka nje.

Tutuba alitoa kauli hiyo jana jijini Arusha alipofungua semina ya siku tatu ya wahariri wa vyombo vya habari iliyoandaliwa na Wizaya ya Fedha na Mipango.

Alisema kuwa kutokana na sifa ya kukopesheka, serikali inaendelea kutunza heshima hiyo ili iendelee kuaminika.

Tutuba alisema mikopo ya serikali inatoka kwa awamu tofauti na kila muda wa kurejesha deni unapofika, serikali imekuwa ikirejesha kwa wakati mkopo pamoja na riba kulingana na matakwa ya mkataba.

"Hapa kwenye Deni la Taifa nimeona niwatoe wasiwasi Watanzania kwa sababu serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imekuwa ikilipa Deni la Taifa kwa wakati kulingana na matakwa ya mkataba wa fedha zilizokopwa," alisema.

Kuhusu akiba za fedha za kigeni walizojiwekea kwenye nchi za EAC, alisema Tanzania ina akiba ya zaidi ya miezi sita kwa ajili ya kuagiza bidhaa toka nje ya nchi kwa kipindi hicho.

"Tulijiwekea utaratibu huu wa kuweka akiba ya fedha za kigeni ili tuwe na uhakika wa kuwa na fedha za kutuwezesha kuagiza bidhaa toka nje," alisisitiza.

Kuhusu mfumuko wa bei, Katibu Mkuu alibainisha kuwa hadi kufikia Februari mwaka huu, ulikuwa umepungua hadi asilimia 3.7 toka zaidi ya asilimia nne Januari mwaka huu.

"Shilingi yetu inaendelea kuimarika ambapo kwa sasa mfumuko wa bei wa bidhaa mbalimbali nchini upo chini ya asilimia tano huku uchumi ukiendelea kuimarika," alisema.

Tutuba alisema katika kusimamia miradi ya maendeleo, serikali imetumia zaidi ya Sh. trilioni 8.4 hadi kufikia Februari mwaka huu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Kati yake, Sh. trilioni 6.2 ni fedha za ndani na Sh. trilioni 2.2 ni fedha za nje.

Alisema kuwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo, serikali ilianzisha mfumo wa utumiaji wa mafundi jamii (Force Account) ili kupunguza gharama za kutekeleza miradi katika maeneo mbalimbali nchini.

"Mfumo huu unapunguza gharama za ujenzi wa miradi ambapo taasisi na mashirika ya serikali yanapewa fedha za kutekeleza miradi katika maeneo yao, wananunua vifaa vyote na kuwatumia mafundi wa kawaida kujenga miradi hiyo na imetekelezeka kwa ufanisi mkubwa," alisema.

Katibu Mkuu alisema mfumo huo unakuwa na kamati ya usimamizi, ununuzi wa vifaa na mapokezi, lengo kubwa kuweka kamati hizo likiwa ni kuzuia mgongano wa maslahi.

Kwa mujibu wa Tutuba, serikali inaendelea kutekeleza miradi mingi midogo na mikubwa, ikiwamo ya kimkakati, kwa kutoa fedha kwa wakati ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live