Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yashinda rufaa ya makinikia

53652 Pic+makinikia

Tue, 23 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Bodi ya Rufaa za Kodi (Trab) imebariki uamuzi wa Serikali kuyashikilia na kuzuia kusafirishwa nje ya nchi makontena ya mchanga unaodaiwa kuwa na madini maarufu kama makinikia, yanayomilikiwa na kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Bulyanhulu Gold Mine (BGM).

Novemba 29, 2017, BGM ilikata rufaa Trab dhidi ya kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) ikipinga kukamatwa makontena yake 104 ya makinikia yanayodaiwa kuwa ya dhahabu.

Ilikuwa ikidai kuwa makontena hayo yaliyokuwa bandarini kwa maandalizi ya kusafiishwa nje ya nchi kwa ajili ya uchenjuaji yalikuwa yameshikiliwa kinyume cha sheria, kwani usafirishaji wa makinikia hayo ni kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Trab katika hukumu iliyotolewa na aliyekuwa mwenyekiti wake, Cyprian Mkeha baada ya kusikiliza rufaa hiyo ilikubaliana na hoja za TRA kupitia kwa wakili wake, Juma Beleko kuwa ilikuwa sahihi.

Katika uamuzi huo wa Trab uliosambazwa kwa wadau Alhamisi iliyopita imekubaliana na wakili Beleko kuwa makinikia yaliyokamatwa ni miongoni mwa bidhaa zilizozuiwa kwa mujibu wa kanuni za uchimbaji madini (Biashara ya Madini) chini ya kifungu cha 211 cha Sheria ya Uchimbaji Madini.

Bodi hiyo inayofanya kazi kama mahakama yenye dhamana ya uamuzi wa kesi za kodi, hatua ya awali inasema kuwa kifungu cha 3 (1) cha Sheria ya Uchimbaji Madini kinazuia usafirishaji madini yoyote nje ya nchi bila ya kibali.

Imesema BGM haikuonyesha ushahidi kama ilikuwa na kibali cha usafirishaji wa makinikia katika makontena yaliyokamatwa.

“Alikuwa (kamishna mkuu TRA) na mamlaka chini ya kifungu cha 216 (2) cha Sheria ya Usimamizi wa Shughuli za Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuendelea kushikilia bidhaa zilizokamatwa ni miongoni mwa zilizozuiwa,” inasema Trab katika hukumu hiyo.

“Kuendelea kushikilia na kuziweka kizuizini bidhaa zilizokamatwa ni halali. Kwa kusema hivyo kwa kauli moja tunaamuru kuwa rufaa haina mashiko. Hivyo inatupiliwa mbali yote.”

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, mgogoro huo ulianza Machi 3, 2017, katibu mkuu wa Wizara Nishati na Madini alipotoa taarifa ya zuio la usafirishaji nje mchanga wa madini yenye asili ya metali na hivyo Serikali ilipiga marufuku usafirishaji nje makinikia na madini.

Hata hivyo, Julai 20, 2017, makontena 104 ya makinikia ya BGM yalikamatwa bandarini na kamishna mkuu wa TRA katika taarifa yake kwa BGM alitoa sababu mbalimbali za kukamatwa kwa makontena hayo.

Sababu hizo ni pamoja na kutoa taarifa ya uongo ya usafirishaji kwa kutojumuisha madini ya Rhodium, Iridium Sulphur, Tantalum, Iron, Lithium, Berullium na Tttebium na kutangaza uzito na thamani ya chini ya madini.

Nyingine ni usafirishaji haramu wa makusudi wa madini kinyume cha masharti na kwamba BGM ilifanya hivyo kinyume cha Sheria ya Usimamizi wa Masuala ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kutokana na hoja hizo, kamishna mkuu wa TRA chini ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi aliitaka kampuni hiyo kuwasilisha ushahidi wa taarifa mbalimbali.

Ushahidi huo ni hati halisi ya au iliyothibitishwa ya malipo mrabaha iliyoandaliwa na kusainiwa na mrufani, kutathmini na kulipa ada ya mrabaha wa madini mengine zaidi ya dhahabu, shaba na fedha yaliyomo katika makontena 277 ya makinikia yaliyokuwa katika maghala yakisubiri kusafirishwa.

Vilevile risiti halisi au iliyothibitishwa ya malipo taslimu iliyotolewa kwa mrufani kuhusu malipo ya mrabaha wa madini mengine zaidi ya dhahabu, shaba na fedha yaliyokuwemo kwenye makontena hayo.

Pia, kibali cha kusafirisha nje madini mengine zaidi ya dhahabu, shaba na fedha yaliyokuwemo na fomu halisi au iliyothibitishwa ya maombi ya kusafirisha nje ya nchi madini mengine zaidi ya dhahabu, shaba na fedha yaliyokuwemo.

Vilevile aliomba nyaraka za tamko la kusafirisha nje ya nchi na kuhusu uzito wa makontena 277 ya makinikia kabla na baada ya kufungwa, na taarifa nyingine ambazo mrufani angeona kuwa ni muhimu kuthibitisha usafirishaji.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, BGM ilidai kamishna aliyakamata na kuyazuia makontena hayo kinyume cha sheria kwani hakutimiza masharti ya Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hivyo ilidai kamishna hakuwa na mamlaka ya kuomba hati mbalimbali za ushahidi ilizoziomba kutoka kwa mrufani huku ikisisitiza kuwa bidhaa hizo zilipaswa kuachiliwa na kwamba si miongoni mwa zilizozuiwa.

Wakili Beleko akijibu hoja hizo alidai kuwa kifungu cha 2 na cha 70(2) vya Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kanuni (Biashara ya Madini) Uchimbaji wa Madini za mwaka 2010, vinabainisha kuwa madini ni bidhaa zilizozuiwa. Alidai kuwa chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kamishna mkuu TRA ana mamlaka ya kudhibiti usafirishaji wa bidhaa nje.



Chanzo: mwananchi.co.tz