Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yashauriwa kuwekeza teknolojia sekta ya Kilimo

Kilimo Kilimanjaro Serikali yashauriwa kuwekeza teknolojia sekta ya Kilimo

Wed, 30 Nov 2022 Chanzo: mwanachidigital

Kama ilivyo kwa watumiaji wa 3G katika Dunia iliyofikia mageuzi ya 5G ndivyo ilivyo kwa Tanzania kuwa nyuma katika matumizi ya teknolojia hususani katika sekta ya kilimo.

Kauli hiyo inaakisi matokeo ya utafiti unaotokana na takwimu za machapisho ya uwekekezaji wa teknolojia katika sekta kilimo kati ya 2006 hadi 2021 kwa upande wa mataifa ya Afrika.

“Matokeo yanaonyesha Tanzania bado tunakabiliwa na changamoto ya matumizi ya teknolojia, wenzetu walioendelea wako mapinduzi ya nne, sisi bado tuko mapinduzi ya tatu,” amesema Profesa Edda Luoga, Naibu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), upande wa taaluma, utafiti na ushauri wa kitaaluma.

Profesa Luoga ametoa kauli hiyo leo Novemba 29, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa wasilisho lake katika kongamano la kwanza la Kimataifa chini Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA).

Katika ufafanuzi wake Profesa Luoga amesema licha ya matumizi ya simu na intaneti kuongezeka nchini, mataifa makubwa yamejiimarisha kwenye ushindani wa matumizi mengine ya Tehama.

Baadhi ya hayo ni matumizi ya teknolojia ya akili isiyo asilia (artificial intelligence), mashine za kisasa za kuvuna na kupembua nafaka, matumzi ya Robot.

Matumizi mengine aliyosisitiza ni sarafu mtandao kwa ajili ya kulipia bidhaa na takwimu zinazosaidia uhakika wa mazao ya kulima na masoko na teknolojia ya kutengeneza vitu kwa kutumia kichapishi cha 3D.

“Kwa hiyo tunaitaji kuwekeza katika teknolojia hizo ili kuongeza tija katika uzalishaji na mchango wa sekta hiyo kwa Taifa,” amesema.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uchumi na uwekezaji), Mudrik Soraga aliyekuwepo katika kongamano hilo, amesema serikali itakuwa tayari kupokea na kufanyia kazi utafiti unaotafuta majibu ya changamoto zilizopo.

“Zimewasilishwa ripoti kadhaa, ninaahidi kuwa balozi wa kushawishi ili zifanyiwe kazi. Zaidi tunatakiwa kujikita katika tafiti zinazozalisha ajira nyingi hususani kilimo ambayo tunatakiwa kuboresha zaidi,” amesema Soraga.

Kongamano hilo limehusisha watafiti, wahadhiri, wanafunzi na watunga sera kwa lengo la kujadili nafasi ya ubunifu, uvumbuzi na uwekezaji katika kuchochea maendeleo endelevu.

Katika kongamano hilo linaloendelea hadi jioni saa 11, limehusisha uwasilishaji wa ripoti zaidi ya 10 zilizojikita kushauri eneo la uwekezaji katika ubunifu na uvumbuzi nchi za Afrika ikiwamo Tanzania.

Naye Profesa Suleiman Nasiru, Mkuu wa Idara ya tafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia nchini Ghana, amewasilisha ripoti yake inayoonyesha umuhimu wa kuwekeza katika sekta ya elimu na afya ili kuzalisha nguvu kazi yenye tija katika maendeleo endelevu.

Chanzo: mwanachidigital