Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yashauriwa kufungua milango kwa wawekezaji

51813 Repoa+pic

Thu, 11 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ili Watanzania waweze kupata maendeleo ya kiuchumi, Serikali haina budi kufungua milango kwa wawekezaji na kuruhusu ukuaji na ustawi wa biashara.

Hayo yamebainishwa na wadau wa maendeleo leo Alhamisi Aprili 11, 2019 wakizungumza katika warsha ya 24 ya taasisi ya utafiti ya Repoa iliyokuwa ikijadili maendeleo ya uchumi wa ndani ngazi ya chini na namna ambavyo Tanzania inaweza kunufaika na mfumo huo.

Ofisa Mtendaji wa Kampuni ya Ushauri wa Fedha na Uwekezaji wa SSC Capital, Salum Awadh amesema kuna vikwanzo katika urasimishaji  biashara nchini jambo linalokwamisha maendeleo na kuathiri ukusanyaji kodi za Serikali.

"Huu si wakati sahihi wa kuwa na mamlaka nyingi zinazosababisha urasimu katika ufunguaji biashara. Huu sio wakati wa kuwa na kodi nyingi za kero, kadri biashara inavyoathirika ndivyo mapato ya kodi yanavyopungua na soko la ajira linavyoathirika," amesema Awadh.

Amesema uchumi shirikishi unaanzia serikali za mitaa, biashara zisizo rasmi zinapaswa kurasimishwa na ulipaji kodi uwe rahisi zaidi ili kuwavutia watu wengi kulipa kwa wakati.

 

Waziri wa Viwanda, Biashara na Utalii wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali amesema ubunifu ni muhimu katika maendeleo ya Tanzania kwa kuwa hutatua changamoto zinazoikabili jamii lakini kama nchi inapaswa kuruhusu ushamiri kwa biashara.

"Tunaweza kufanya vizuri na kuinua uchumi wa watu, hii itawezekana kama tukiruhusu kukua kwa biashara na kuwafanya wawekezaji wetu wajivunie kuwekeza kwetu," amesema Balozi Amina.

Alisema mikoa inapaswa kushirikiana na kuelezana fursa zilizopo katika maeneo yao akitolea Zanzibar, kuwa sasa chaki zinazotumika shuleni zinatoka Simiyu kabla ya hapo zilikuwa zinanunuliwa nchi za nje.

"Serikali za mitaa zinaweza kutengeneza fursa kwa watu wake kwa kutangaza mambo yaliyopo katika eneo hilo, mfano Zanzibar inatumia tani 100,000 za mchele. Awali zilikuwa zinatoka China na Pakstani lakini nilipotembelea Simiyu nilibaini wana uwezo wa kusambaza mchele nusu ya mahitaji yetu vilevile chaki," amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz