Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yasaka eneo la kuuzia samaki Kasanga

D4b49800975f7cd965865e3c3a0c0fac Serikali yasaka eneo la kuuzia samaki Kasanga

Tue, 11 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imesema inasaka eneo maalumu kwa ajili ya ujenzi wa soko la muda la kuuzia samaki katika Kata ya Kasanga iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji cha Ziwa Tanganyika.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi, Dk Rashid Tamatamahm alibainisha hatua hiyo jana baada ya kutembelea eneo hilo na kujionea uharibifu wa miundombinu ya soko la sasa kufunikwa na maji.

Alisema wizara inatafuta eneo la muda huku ikitafakari pia mipango ya muda mrefu ya kujenga sehemu ambayo ni salama zaidi.

“Kwa hali ilivyo hapa, na jinsi nilivyoiona, hatuwezi kufanya chochote hapa, nitamshauri waziri tutafute eneo lingine na tutenge fedha za kujenga mwalo (soko) mwingine, tutafute eneo ambalo litafanyiwa tathmini, hata maji ya ziwa yakiongezeka kusitokee athari ya namna hii,” alisema.

Katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2020/21 inayoishia Juni mwaka huu, wizara ilikuwa imetenga Sh milioni 78 kwa ajili ya ukarabati mdogo katika Soko la Kasanga, Sh milioni 748 katika Soko la Kirando lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa na Sh milioni 187 katika Soko la Muyobozi lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Hata hivyo ukarabati ulishindwa kufanyika katika masoko hayo kutokana na kina cha maji cha Ziwa Tanganyika kuongezeka na kuanza kusababisha athari.

Alisema Soko la Kasanga lilianza kutumika Machi mwaka jana ambapo uwekezaji wake umegharimu zaidi ya Sh bilioni 1.3, ikiwa ni gharama ya miundombinu na vifaa vilivyowekwa na serikali na wadau wakiwemo Umoja wa Ulaya (EU).

Aidha, alisema kwa sasa hakuna sehemu maalumu ya kushushia samaki, hali inayowalazimu kushushia maeneo yasiyo na ubora.

Alisema kukosekana kwa soko la kuuzia samaki katika Kata ya Kasanga, kumesababisha kuwapo kwa biashara ya samaki kwa kutumia njia zisizo rasmi ikiwemo ya kupeleka Zambia baada ya kukosekana kwa soko.

Ofisa Mfawidhi Msimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda Kuu ya Tanganyika, Juma Makongoro, aliwataka wananchi wanaotaka kuuza samaki nchini Zambia, kufuata utaratibu kwa kuwahusisha watu au kampuni zenye leseni za kusafirisha samaki kwenda nje ya nchi ili waweze kuuza samaki kwa njia halali.

Chanzo: www.habarileo.co.tz