Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaridhishwa viwango bidhaa za wanawake wajasiriamali

D04ca2e14b64711a7cda08a84e17d33b.jpeg Serikali yaridhishwa viwango bidhaa za wanawake wajasiriamali

Sun, 6 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imeridhishwa na hatua ya wanawake wengi wajasiriamali wanaoshiriki Maonesho ya Pili ya Bidhaa za Wanawake Wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali nchini kuwa na bidhaa zenye viwango, hivyo kuwa fursa nzuri ya kuimarisha uchumi wa familia zao.

Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, wakati akifungua Maonesho ya Pili ya Bidhaa za Wanawake Wajasiriamali yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

Jafo, alilipongeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kazi nzuri na kulitaka shirika hilo kusaidia vikundi vya akinamama ili viweze kuratibiwa vizuri.

Alisema baadhi ya wanawake wana changamoto mbalimbali na wengine hawajapata alama ya ubora ya TBS, hivyo alitoa mwito kwa wadau wote wanaoshughulika na wanawake wajasiriamali kuhakikisha wanaondoa vikwazo kwa akinamama hao ili waweze kusonga mbele.

"Kwa nilichokiona sasa naamini sasa mpo vizuri na hii ina maana kwamba wanawake wakijenga uchumi watasaidia sana kuimarisha familia zao na hivyo kuwa na maisha bora zaidi," alifafanua.

Awali akizungumza na waandishi wa habari, Ofisa Udhibiti Ubora wa TBS, Amiti Msanjila alisema wameshiriki maonesho hayo kutokana na wao kuwa wadau wakubwa katika kuwezesha biashara kwa lengo la kuwapatia elimu washiriki kuhusiana na namna ya kupata alama ya ubora, usajili wa bidhaa za vipodozi pamoja na vyakula.

Alisema TBS imekuwa ikitoa alama ya ubora kwa wajasiriamali bure, hivyo ili waweze kuhudumiwa na shirika hilo wanatakiwa kuwa na barua ya utambulisho kutoka SIDO na mtaji wao uwe chini ya milioni 70.

Kuhusu faida ya alama ya ubora kwa bidhaa, Msanjila alisema inaogoza imani kwa umma kwamba bidhaa zao ni salama na zinakidhi matakwa ya viwango, hivyo zinaweza kufanyakazi iliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Meneja wa Mawasiliano ya Umma na Masoko wa TBS, Gladness Kaseka, alisema maonesho hayo ni fursa nzuri kwa shirika hilo kukutana na washiriki 400 na kufikisha ujumbe kuhusiana na mpango wa shirika kuthibitisha bure bidhaa za wajasiriamali.

Alifafanua kwamba kila mwaka serikali inatenga zaidi ya Sh milioni 200 kuhudumia wajasiriamali wadogo, hivyo kupitia maonesha hayo wameweza kupata fursa ya kuzungumza nao, kuwatembelea kwenye mabanda yao kusikiliza changamoto zao na kuwaelekeza hatua ambazo wanaweza kuchukua kuzipatia ufumbuzi.

Kikubwa ambacho shirika hilo limejivunia kwa mujibu wa Kaseka ni kuona wajasiriamali wengi wanaoshiriki maonesho hayo kuthibitisha usalama na ubora wa bidhaa zao.

Maonesho hayo yalioanza Machi 3, mwaka huu yameandaliwa na Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC). Yanatarajiwa kumalizika Machi 8, mwaka huu, Siku ya Wanawake Duniani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live