Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yapongezwa kukubali PPP bandari Dar

Bandari Tanga Tangaaa Serikali yapongezwa kukubali PPP bandari Dar

Mon, 29 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WADAU wa masuala ya uchumi wameipongeza serikali kwa kukubali kuishirikisha sekta binafsi kuendesha Bandari ya Dar es Salaam.

Hivi karibuni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alilieza Bunge kuwa ni lazima kushirikisha sekta binafsi kuiendesha bandari hiyo.

Profesa Mbarawa alisema hayo bungeni Dodoma wakati anajibu hoja za wabunge waliochangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Profesa Mbarawa aliwaeleza wabunge kuwa kampuni yenye sifa hizo itakapopatikana itapunguza muda wa meli kushusha mizigo kutoka siku tano hadi saa 24, kuongeza meli zinazokuja Bandari ya Dar es Salaam na itapunguza muda kushusha makasha kutoka siku nne hadi siku moja na nusu.

“Suala la uwekezaji binafsi halina mjadala tunakwenda kuruhusu,” alisema.

Mtaalamu wa Uchumi, Dk Donald Mmari alisema serikali imefanya uamuzi sahihi kwa kuwa sekta binafsi ndiyo mfanyabiashara anayelenga kutengeneza faida.

Dk Mmari alisema ili ushirikishwaji huo uwe na tija ni lazima mkataba uwe wa wazi, uweke wazi kuhusu mapato pamoja na kuruhusu ukaguzi wa hesabu na ununuzi wa vifaa vya kazi.

“Mfano mzuri ni Uholanzi, shughuli zote za bandari zinafanywa na sekta binafsi serikali inatoa usimamizi pekee.

“Hatua hii itaongeza bishara zaidi, ufanisi utaongezeka, sekta zingine zitaimarika na kupunguza rushwa kwa asilimia kubwa,” alisema.

Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Dk Isack Safari alisema uamuzi huo ni mzuri kwa sababu sekta binafsi ina sifa ya kupambana kutengeneza faida.

Dk Safari alisema sekta binafsi itatumia teknolojia rahisi kurahisisha kazi hali inayofanya itumie gharama kidogo kutengeneza fedha nyingi kama vile matumizi ya vifaa vya kisasa pamina na matumizi ya teknolojia zaidi badala ya rasilimali watu hali inayopunguza matumizi.

“Ndani ya bandari kuna makampuni binafsi na yanafanya kazi vizuri hususani katika kupakia na kupakua mzigo hali iliyoifanya Benki ya Dunia kuitaja Bandari ya Dar es Salaam ya kwanza Afrika Mashariki kwa utoaji wa huduma,” alisema.

Mchambuzi wa Uchumi, Profesa Wetengere Kitojo alisema sasa ni wakati wa Bandari ya Dar es Salaam kufahamika duniani kwa sababu sekta binafsi ndiyo inayoweza kufanya biashara na si serikali.

“Serikali haipo kwa ajili ya kufanya biashara, mahali ilipojaribu kufanya biashara ulifeli lakini kwa sekta binafsi ndio penyewe,” aliongeza Profesa Kitojo na kuongeza kuwa uamuzi huo unaweza kusaidia kumaliza tatizo la rushwa bandarini.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga aliishukuru serikali kwa kuishirikisha sekta binafsi katika kuendesha bandari na kuongeza kuwa nia ya sekta binafsi ni kuifikisha bandari katika nafasi ya 100 bora kutoka nafasi ya 312 ilipo sasa hivi.

“Ushirikishwaji wa Sekta binafsi utaongeza ufanisi katika utendaji kazi wa bandari pamoja na kuongeza ujuzi na kuweza kuwekeza kwenye miundombinu ya bandari ili serikali itumie fedha ambazo zingeweza kutumika kwenye miundominu hii kufanya shughuli nyingine za kuleta huduma kwa jamii,” alisema Maganga.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live