Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yapewa ushari kuepuka hasara ATCL

Atcl Pic Data Serikali yapewa ushari kuepuka hasara ATCL

Mon, 17 Apr 2023 Chanzo: Habarileo

WACHAMBUZI wa masuala ya uchumi wameishauri serikali itoe upendeleo maalumu kwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ili kuiongezea mapato na kuiepusha na hasara.

Wametaja miongoni wa upendeleo huo ni kuipata fursa ATCL itoe huduma katika viwanja vya ndege na ndani ya ndege zake.

Wamepinga wazo la kuimilikisha ATCL ndege zinazomilikiwa na Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) kwa madai kuwa hicho si kigezo cha kuifanya ipate faida.

Mchambuzi Bubelwa Kaiza alisema hoja ya ATCL kumilikishwa ndege si ya kiuchumi kwa kuwa hakuna biashara yoyote ya kiuchumi ambayo anataka apate faida tu bila kudaiwa.

Kaiza alisema faida na hasara haihusiani na kudaiwa au kutodaiwa kwa kuwa mtu anaweza kudaiwa na bado akatatengeneza faida kubwa kwenye biashara yake.

“Kinachotakiwa ATCL ni kuwa na mkakati wa kufanya shughuli zao za kibiashara, ndege iwe wamekodisha au wamenunua siyo hoja, tatizo ni kwamba hawana huo mkakati wa kibiashara na pengine hata mkataba wa kukodisha ndege baina yao na serikali haupo sawa sawa,”alisema.

Kaiza alisema duniani kote mashirika mengi yanakodisha ndege na bado yanapata faida, hivyo hoja ya kuwamilikisha ndege ATCL kwamba watapata faida siyo mawazo ya kibiashara wala kiuchumi bali ni mawazo yasiyofaa na kwenye uchumi hakuna kitu kama hicho.

“Madeni hayajawahi kuleta hasara kama una mpango mzuri wa biashara, kila kampuni kubwa, shirika kubwa huwa wanakopa mabilioni ya pesa benki yanafanya biashara, yanapata faida na yanalipa madeni, deni likiisha wanatafuta madeni mengine ili waogeze ukubwa wa biashara,”alisema.

Aliongeza “Kama itaimilikisha ndege ATCL, serikali itapata hasara zaidi kwa sababu wanaweza kubweteka, hasara ya ATCL haiko kwenye kukodishwa au kuazimwa ndege, bali kwenye mkakati wao wa biashara.”

Alishauri bodi ya ATCL isiwe ya kuteuliwa na iundwe kamati maalumu au mamlaka maalumu ya kuajiri wajumbe wa bodi ambao wataomba kazi, wapatikane kwa ushindani na wapewe malengo ya kuyafikia ya kila mwaka.

Mchambuzi Gabriel Mwang’onda alisema kumiliki ndege ni gharama na ndiyo maana mashirika mengi ya ndege hayanunui ndege kwa sababu gharama ya kununua ndege moja inaweza kufika dola milioni 300, dola milioni 200 au dola milioni 70 ambazo ni fedha nyingi.

“Mashirika mengi ya ndege yanayojiendesha kibiashara hayanunui ndege bali yanakodi ndege kwa sababu kazi yao siyo kumiliki ndege bali ni kutengeneza mapato, na mapato yanatengenezwa kwa kusafirisha mizigo au abiria na kutoa huduma nyingine,”alisema Mwang’onda.

Kuhusu huduma hizo nyingine, alisema serikali inapaswa kutoa upendeleo maalumu kwa ATCL ili itengeneze faida kwa kuhakikisha huduma zote katika viwanja vya ndege vya ndani wanapewa ATCL.

Alizitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na kupakia na kushusha mizigo kwenye ndege, huduma za uhandisi kwenye ndege zote zinazokuja nchini, huduma za kukagua abiria wanaoondoka na wanaowasili, eneo la kukaa abiria wanaotaka kuondoka au wanaowasili pamoja na huduma za chakula ndani ya ndege za ATCL.

Mwang’onda alisema mashirika makubwa ya ndege yakiwemo yanayokuja nchini yanatengeneza faida kwa sababu ya upendeleo wanaoupata kutoka kwa serikali zao kwa kutoa huduma hizo kwenye viwanja vya ndege.

“Sekta ya ndege kwenye nchi husika haitakiwi kuwa huria inabidi iwe ya upendeleo, unatoa upendeleo mahususi kwa ndege yako, pale kiwanja cha ndege kampuni zinazotoa huduma zinatakiwa ziwe za ATCL kwa kuwa kampuni hizo zinatengeneza hela nyingi kuliko hata ndege,”alisema.

Aliongeza “Huduma za namna ile kwa nchi nyingine hawawezi kuzipa kampuni za nje, zinawapa kampuni ya ndege ya nchi, fedha zinabaki nchini, kupeleka mizigo kwenye ndege, kupokea watu wanaofika, kukagua watu wanoondoka, kusafisha ndani ya ndege, kazi hizi zina hela nyingi, kufanya hivyo kwa ndege moja, gharama yake inazidi dola 50,000, wahandisi kukagua tu ndege dola 15,000, sasa ukiwapa kazi hii ATCL watapata faida kubwa.”

Chanzo: Habarileo