Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yapewa somo kuboresha utalii wa utamaduni

Mon, 18 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wadau wa utalii wamesema kuna haja ya Serikali kuwekeza zaidi kwenye utalii wa utamaduni kwa maelezo kuwa unakuwa kwa kasi na unaweza kuongeza idadi kubwa ya watalii na kuchangia zaidi pato la Taifa.

Kwa sasa utalii wa wanyamapori na fukwe ndio unaongoza zaidi nchini Tanzania, lakini kuna utalii wa utamaduni ambao unachochewa na uwepo wa makabila zaidi 120 ambayo yanapatikana nchini huku watalii wakipenda kujua undani wake.

Taarifa kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) zinaonyesha utalii huo utatengeneza zaidi ya ajira 50,000 ifikapo mwaka 2022 kupitia mradi wa miaka mitano unaolenga kuboresha utalii wa utamaduni nchini.

Pia, kwa mujibu wa utafiti unaofanywa kila mwaka na Shirika la Unated Nations- World Toursim Organisation (UN-WTO) unaonyesha utalii wa utamaduni unakuwa kwa kasi kubwa duniani hususani barani Afrika.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Utalii, Richard Rugimbana wakati wadau wa sekta walipokutana kujadili sera ya utalii.

“Tanzania pekee barani Afrika ndio tumebarikiwa utajiri wa utamaduni, hapa tunatakiwa wadau pamoja na Serikali tuwajengee uwezo vikundi vya kikabila vitu ambavyo vitavutia zaidi watalii," amesema.

Amesema  katika mkutano wao wataangalia mambo matatu, “Kwa hapa kwetu utalii mkubwa ni ule wa vyanzo vya asili kama mbuga, milima na maji.”

Amebainisha kuwa ajenda ya pili itakuwa ni utalii wa utamaduni, kwamba hili limetiliwa mkazo kwenye sera  kwa lengo la kuliendeleza kwa maelezo kuwa  Tanzania ina makabila mengi, “Kila Mkoa una fursa ya kuendeleza utalii kupitia utalii wa utamaduni.”

Amesema jambo la tatu ni jinsi gani Watanzania wanaweza kushirikishwa na kuendeleza utalii na kuanza kuwa watalii na kuwekeza katika utalii wa ndani.



Chanzo: mwananchi.co.tz