KATIKA kipindi cha Mwaka 2019/20 hadi 2020/21, serikali imewekeza Sh bilioni 5.8 kuendeleza zao la chikichi nchini.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Assa Nelson Makanika (CCM),
Makanika alitaka kujua kama serikali haioni umuhimu wa kuwekeza katika zao la mchikichi badala ya kuziachia halmashauri ili kukabiliana na upungufu wa mafuta nchini.
Naibu Waziri Bashe alisema hadi kufikia Januari 31, 2021, miche bora ya michikichi 2,244,935 ilikuwa imezalishwa na miche 1,456,111 imesambazwa kwa wakulima katika halmashauri za wilaya za Mkoa wa Kigoma.
“Miche 788,824 inatarajiwa kusambazwa kwa wakulima katika msimu wa 2020/2021,” alisema.Aidha, katika mwaka 2021/22, serikali imetenga Sh bilioni 3.15 kuzalisha na kusambaza mbegu na miche ya michikichi.
Alisema hatua hiyo inalenga kupunguza upungufu wa mafuta ya kula nchini, kwa kuwa hadi sasa, mahitaji ya mafuta ya kula nchini yanakadiriwa kuwa tani 570,000 kwa mwaka.
"Hata hivyo, uzalishaji wa mafuta ya kula nchini unakadiriwa kufikiwa wastani wa tani 205,000 na kufanya upungufu wa wastani wa tani 365,000 kwa mwaka," alisema.
Bashe alisema kutokana na upungufu huo, nchi inalazimika kutumia wastani wa Sh bilioni 474 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi kwa mwaka.
"Kama ilivyo kwa mazao mengine, serikali huwekeza katika utafiti, uzalishaji na upatikanaji wa pembejeo za kilimo, huduma za ugani, udhibiti wa visumbufu vya mazao na utafutaji wa masoko," alisema.
Aidha, katika utekelezaji mikakati hiyo, serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo mamlaka za serikali za mitaa na sekta binafsi.
Alisema kama sehemu ya mkakati wa kujitosheleza kwa mafuta ya kula, mwaka 2018 Serikali iliamua kuanzisha Kituo cha Utafiti wa zao la michikichi cha TARI- Kihinga mkoani Kigoma ili kuendeleza zao hili kwa ufanisi zaidi.
Alisema, TARI-Kihinga inashirikiana na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), halmashauri na sekta binafsi katika utafiti, uzalishaji wa miche bora ya michikichi na kuisambaza kwa wakulima.
Kwa mujibu wa Bashe, serikali itaendelea kushirikisha wadau wa sekta ya umma na binafsi kuendeleza zao la mchikichi na mazao mengine ya mbegu ili kuwezesha nchi kujitosheleza kwa mafuta ya kula.
Aidha, mamlaka za serikali za mitaa zinashauriwa kuwekeza katika mazao ya kilimo kutokana na mapato yatokanayo na ushuru wa mazao likiwemo zao la michikichi.